OKWI, KAGERE, WAWA WAMKUNA KOCHA SIMBA

NA MWANDISHI WETU


 

KOCHA wa viungo wa Simba, Mtunisia Adel Zrane, ameweka wazi jinsi anavyokunwa na wachezaji Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Pascal Wawa, kwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaokwenda sawa na mazoezi yake.

Kocha huyo aliyetua Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja kutokana na pendekezo la Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems, aliliambia BINGWA jana kuwa, mazoezi yake huwa anayagawa katika makundi matatu.

Alisema kuwa, makundi hayo hupangwa kulingana na maeneo husika, yaani viungo, mabeki na fowadi, ili kumpa urahisi wa kila kundi kuwapa mazoezi yake kabla ya kuwachanganya katika mazoezi ya pamoja.

Alisema katika eneo la mabeki, Wawa amekuwa akifanya vizuri zaidi, kwani kila zoezi analotoa, raia huyo wa Ivory Coast huwa analifanya kwa kulitendea haki, licha ya wengine pia kufanya kama anavyotaka.

Zrane aliongeza kuwa, katika eneo la ushambuliaji, Okwi na Kagere wanalingana katika utendaji wao mazoezini na mara nyingi wamekuwa wakienda sawa, huku eneo la viungo, takribani wote wakifanya vizuri.

“Huwa nawapa mazoezi tofauti kulingana na maeneo yao, nikiwagawa katika makundi matatu yaani, eneo la ushambuliaji, beki na viungo, hii inanipa wepesi wa kufahamu uwezo wa kila eneo na zoezi husika,” alisema Zrane.

Zrane, ambaye amechukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa viungo wa timu hiyo, Aymen Hbib,  aliyekuwa pamoja na Mfaransa, Pierre Lechantre, aliyeondoka baada ya mkataba wake na Simba kumalizika, aliungana na kikosi cha Simba walipokuwa kambini nchini Uturuki walikokwenda kujiandaa na msimu huu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*