googleAds

OKWI, KAGERE HAKUNA KULALA

NA ZAITUNI KIBWANA

Washambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na Adam Salamba, wamepewa kazi maalumu ya kuhakikisha hawapotezi nafasi za kizembe kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa kesho dhidi ya African Lyon.

Mastraika hao wakiwa na wenzao, wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterans, Dar es Salaam kujiandaa kuichakaza Lyon katika mchezo huo wa raundi ya saba utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema kikosi hicho kinaendelea kujifua kwa ajili ya mchezo huo wa kesho, huku wakiwa na nyota wao wote, isipokuwa wanne tu waliopo timu ya Taifa, Taifa Stars.

“Wachezaji wote wapo kambini, tunaendelea na programu, hata Okwi, Kagere hawajaondoka, tupo nao bado tunaendelea na programu kama kawaida,” alisema.

Alisema nyota pekee ambao hawapo kikosini mwao ni Jonas Mkude, Aishi Manula, Shomari Kapombe na John Bocco waliopo timu ya Taifa inayojiandaa kuifuata Cape Verde katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2019) zitakazopigwa nchini Cameroon mwakani.

Wakati Masoud akiyasema hayo, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, alisema ana kikosi kipana hivyo haoni tatizo kuwakosa nyota hao waliopo Stars.

“Tunafanya maandalizi ya kutosha ili timu iweze kubadilika na kucheza vizuri zaidi na hatimaye tuweze kupata ushindi kwa kila mechi,” alisema.

Simba iliyokusanya alama 11 katika mechi zake sita, ikishinda tatu, sare mbili na kupoteza moja, itavaana na Lyon iliyopo nafasi ya 16 baada ya kukusanya pointi sita ndani ya michezo saba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*