NYOTA WATATU WASAINI AZAM

NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa Azam umefanikiwa kuingia mkataba na wachezaji watatu, beki wa kati,  Yakubu Mohammed, kiungo mkabaji, Stephan Kingue Mpondo na winga, Joseph Mahundi, kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa mwakani.

Wachezaji hao walisaini mikataba mbele ya baadhi ya viongozi wa klabu hiyo wakiwamo Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Meneja wa timu, Phillip Alando.

Mohammed alisaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Aduana Stars ya Ghana, akiziba nafasi ya Pascal Wawa, huku Mpondo anayetokea Coton Sports ya Cameroon, akisaini mwaka mmoja.

Nyota hao wawili wamepewa rasmi mikataba,  baada ya kulivutia benchi la ufundi la Azam  kwenye majaribio waliyokuwa wakifanya ndani ya kikosi hicho.

Katika kuongeza makali kwenye eneo la ushambuliaji, Azam FC imemrejesha winga wake wa zamani aliyekulia Azam Academy, Mahundi, ambaye amesaini miaka miwili akitokea Mbeya City.

Katika hatua nyingine, Azam imefikia makubaliano ya kuachana na kiungo mkabaji raia wa Rwanda, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, ambaye amepata timu nchini Vietnam na muda wowote kuanzia sasa atakwenda nchini humo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*