NYOTA URUSI ATAMBA KUENDELEZA MOTO WA KOMBE LA DUNIA

MOSCOW, Urusi


 

NYOTA wa timu ya Taifa ya Urusi, Denis Cheryshev, amesema wamepania kuendeleza moto ambao waliuonesha katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika nchini humo, baada ya kuilaza Uturuki kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya UEFA.

Katika mchezo huo ambao ulipigwa mwishoni mwa wiki, ilishuhudiwa mabao yaliyowekwa kimiani na staa huyo na jingine la  Artem Dzyuba yakiwapa ushindi huo na huku yakikihakikishia kikosi cha Kocha  Stanislav Cherchesov kuanza michuano hiyo kwa ushindi.

Mechi hiyo  iliyopigwa mjini Trabzon, ilikuwa ni ya kwanza kwao baada ya kutolewa kwa mikwaju ya penalti na   Croatia katika hatua ya robo fainali, ingawa licha  ya kutoonesha kiwango cha mwanzo, lakini mastaa wake walionekana kujituma muda wote wa mchezo.

Akizungumza mara baada ya mtanange huo, Cheryshev alisema kwa kushirikiana na mwenzake  Dzyuba, watahakikisha wanaipaisha timu hiyo hadi kufikia mbali katika michuano hiyo.

“Bado tunasikitika kutolewa katika hatua ya robo fainali tukiwa nyumbani, lakini sasa tumejipanga ili kuhakikisha tunafika mbali katika michuano hii,” alisema staa huyo.

“Nina uhakika kwa hilo maana bado tuna kiu ya kufanya vizuri na kwa uhakika tutafanya hivyo,” aliongeza staa huyo anayekipiga katika timu ya Valencia na ambaye alifunga bao la kwanza dakika ya 13 ya mtanange huo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*