NYOSSO SI KICHAA WA AKILI

NA CLARA ALPHONCE

JUMATATU wiki hii Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliendelea mzunguko wa 14, ambapo Kagera Sugar waliikaribisha Simba katika Uwanja wa Manispaa wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mchezo huo ulivuta hisia kubwa ya mashabiki hasa wale wa Simba kutokana na matokeo ya mechi ya marudiano ya msimu uliopita iliyochezwa katika uwanja huo.

Katika mchezo huo, Simba walikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji Kagera Sugar na kupoteza malengo yao ya kuchukua ubingwa uliokwenda kwa watani wao wa jadi, Yanga.

Kutokana na matokeo hayo, Simba waliweka nguvu kubwa kuhakikisha hawafanyi makosa msimu huu na kufanikiwa kulipa kisasi kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mara tu baada ya mchezo wa Jumatatu  kumalizika, kulitokea tukio ambalo lilimhusisha beki wa kati wa timu ya Kagera, Juma Nyosso, kumshambulia kwa kipigo shabiki wa soka aliyekuwapo uwanjani kuhushuhudia mtanange huo.

Kitendo hicho kilisababisha Nyosso aondoke na gari tofauti na wenzake walioondoka na basi kwenda kambini na yeye kusindikizwa na askari kwenda kituoni, baada ya shambulio hilo.

Tukio hilo lilizua mjadala mzito kwa wadau na wapenzi wa soka hapa nchini, huku wengi wakihusisha na matukio yake ya nyuma ya utovu wa nidhamu ambayo  yalisababisha kufungiwa kujihusisha na soka kwa  mwaka mmoja.

Ukilichukulia jambo hilo kwa haraka haraka unaweza kuona Nyosso ni mtovu wa nidhamu, lakini mchezaji huyo alichokozwa na kushindwa kujizuia na kuchukua hatua mkononi.

Mashabiki siku zote wamekuwa ni watu wasio na uwezo wa kuzuia hisia zao kiasi cha kutoa lugha chafu kwa wachezaji pindi wanapokosea na kusahau kuwa, wachezaji nao ni binadamu kama walivyo wengine.

Kweli, Nyosso hakutakiwa kuchukua hatua mkononi kumpiga shabiki, lakini wakati mwingine uvumilivu huwa unashindwa na shetani na kuamua  kuchukua maamuzi  mazito bila kujali  matokeo yake.

Nyosso si kichaa wa akili mpaka kufikia hatua ya kupiga watu ovyo, ukweli ni kwamba alichokozwa na yule shabiki alimtolea lugha isiyofaa na alishindwa kuvumilia kama binadamu.

Lakini kwa kuwa alionyesha  utovu wa nidhamu siku nyingi ndio maana anakosa mtetezi kutokana na kosa alilolifanya wiki iliyopita la kumpiga shabiki.

Si tukio la kwanza kwa Nyosso, aliwahi kufanya mengine, lakini kwa hilo la kumpiga lilisababishwa na shabiki mwenyewe.

Mashabiki wakumbuke kuwa wachezaji ni watu wazima wana familia zao, wanahitaji heshima wanapokuwa kazini, pia wanaweza kukosea kama mtu mwingine anavyokosea, hivyo kumtusi  mbele ya wazazi na familia zake si haki.

Miaka ya nyuma, Athuman China, aliyekuwa mchezaji wa Yanga alishawahi kumpiga shabiki jukwaani kwa kosa la kumtukana mama yake mzazi na baadhi ya mashabiki waliokuwepo hapo walimuunga mkono China.

Pamoja na yote, Nyosso pia anahitaji kusaidiwa kisaikolojia kwani matukio hayo ya mfululizo yanahatarisha maisha yake katika soka.

Wataalamu wa kisaikolojia ni muhimu katika timu, kwani kwa kiasi kikubwa wanasaidia kupunguza baadhi ya matatizo makubwa kwa wachezaji.

Kwa mwanasoka ni jambo zuri kuwa timamu kiakili na kimwili, hilo linasaidia  kwa namna moja au  nyingine  kuwa na maamuzi katika mazingira fulani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*