Nyoni atoa siri ya kupindua meza Mkwakwani

NA WINFRIDA MTOI

BEKI wa Simba, Erasto Nyoni, amesema pamoja na kubanwa na Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, lakini maneno ya kocha wao, Patrick Aussems, yaliwapa nguvu na kupindua matokeo.

Katika mchezo huo, ambao Simba walishinda kwa mabao 2-1, kipindi cha kwanza cha mtanange huo kilimalizika wakiwa nyuma kwao bao 1-0, kabla ya kusawazisha na kushinda mchezo huo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nyoni alisema uwanja huo uliwasumbua, lakini kocha aliwaambia watulie wasipige mipira kwa kubutua na mwisho wa siku walifanikiwa kutumia nafasi walizopata.

Alisema Aussems aliwaambia maneno hayo walipokuwa mapumziko, hivyo kurudi uwanjani wakiwa na nguvu mpya.

“Coastal ni timu nzuri kutokana na kuundwa na vijana wengi, lakini kilichotupa changamoto kubwa ni uwanja haukuwa mzuri kwetu, ila mwalimu alituambia tutulie na tusicheze kwa kubutua mipira na kweli tukafanikiwa,” alisema Nyoni.

Alieleza kuwa, wameachana na matokeo hayo, wanachoangalia kwa sasa ni mechi zilizopo mbele yao kuhakikisha wanaendelea kuchukua pointi tatu, ili kutimiza lengo la kutetea ubingwa wao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*