NILISHAKUFA [51]

Ilipoishia

Aliamua kuahirisha kwa siku hiyo kutokana na kujitetea kwangu kulivyoonyesha kuleta ugumu kwenye kesi hiyo. Watu wengi hawakupenda kuahirishwa kwa sababu nilimuua mtu waliyempenda, walitaka hukumu itolewe siku ile ile.

SASA ENDELEA

Tarehe 10 kesi ilisomwa tena, hakimu alitaka nilirudie kuongea yale niliyoyangea siku ile.

Baada ya kurudia maelezo hayo, hakimu aliuliza.

“Mawakili wa upande wa mashtaka mna maswali kwa mshtakiwa?”

“Ndio ndugu hakimu,” alijibu wakili mmoja huku akisimama kwenye kiti.

Wakili huyo wa upande wa mashtaka, alinisogelea kizimbani. Alinitazama sana na kuniuliza.

“Je, marehemu Paulina alimuua mama yako kwa mikono yake?”

Swali hilo lilikuwa gumu kwangu kwa kuwa ni kweli Paulina hakuwa amemuua mama yangu kwa mikono yake na sikuwa na ushahidi wa kuonyesha Paulina alimuua mama yangu. Niliamua kumjibu kulingana na maelezo ya mara ya kwanza na kuongezea mengine katika kujitetea.

“Mama yangu ni mgonjwa wa kichwa, hivyo Paulina alipochukua kila kitu na kuuza hata nyumba wanayoishi, mama yangu alipatwa na mshtuko mkubwa na kupoteza maisha.”

“Jibu rahisi ni kwamba, Paulina hakumuua mama yako na huna ushahidi wa kutosha wa kuieleza mahakama kuwa marehemu Paulina alimuua marehemu mama yako. Hata katika maelezo mengine kwamba alisababisha pia mtoto wa dada yako kufariki bado hatuna ushahidi. Na mara nyingi maelezo kama hayo hayana mashiko mbele ya mahakama kwa sababu, marehemu hakuwagusa hao waliokufa,” aliongea wakili wa mashtaka maelezo yaliyonifanya niendelee kukataa tamaa.

Kujitetea kwangu mahakamani kulikuwa si kwa ajili ya maisha yangu mimi bali ni kwa ajili ya dada na mdogo wangu, sikutaka kukaa kimya bila kujitetea maana ningewavunja moyo zaidi.

Kwa sababu mimi niliamini kuwa mimi ni wa kufa siwezi kuepuka kifo, kifo kilichonitokea siku nyingi, hivyo sikutaka kushindana nacho.

Baadaye alisimama wakili wa pili na kuja kuniuliza maswali.

“Bwana Fredy Olutui, je, una ushahidi wowote wa kuonyesha mbele ya mahakama kuwa mali za marehemu Paulina ni za kwako, nyumba za kifahari magari na vinginevyo?”

Nilibaki kimya kwa dakika moja, swali hilo pia lilikuwa gumu kwangu kwa kuwa pindi nilipoondoka kwenda Uganda, nilikuwa nimeacha kila kitu nyumbani hati za nyumba zangu zote mbili leseni ya biashara ya duka na hati yake ya umiliki. Vyote hivyo alikuwa navyo Paulina, sikuvifikiria sana kwa kuwa nilimwamini.

Jambo lingine ni kwamba, mali nyingine nyingi Paulina alikuwa amezipata baada ya mimi kwenda Uganda, kama vile magari, nyumba mbili za kifahari ikiwemo ile ya kifahari zaidi ya St Kolon. Alizipata kutokana na pesa yangu iliyokuwa benki, sikutaka kuieleza mahakama kuhusu pesa zangu za benki kwa kuwa pesa zile zingeleta maelezo mengine ambayo yangeihusisha Serikali.

Pesa hizo zilikuwa zimetokana na kazi yangu ya upelelezi ndani ya Uganda, kazi iliyokuwa ni ya siri kubwa, ambayo kabla sijaifanya niliapa mbele ya maofisa wa Serikali kuwa sitoisema kwa kuihusisha na kitu chochote.

Sikuwa na ushahidi wa kutosha niliamua kuieleza mahakama kuwa kila kitu nilimwachia mke wangu kwa kuwa nilimwamini. Wakili aliposikia maelezo yangu mafupi alijibu.

“Kwa hiyo huna ushahidi wa kutueleza mahakamani kuwa mali hizo zilikuwa ni zako, ndugu hakimu inaweza kuwa mshtakiwa alitamani mali za marehemu na kuamua kumuua ili azichukue.”

Baada ya kuongea hayo wakili huyo alikwenda kukaa, hakimu aliandika kwenye makaratasi kile alichokiona na kusema.

“Ninawaomba ndugu wa mshtakiwa waje mbele kwa ajili ya kumtetea ndugu yao.”

Aliposema hivyo, dada yangu akiwa anatokwa na machozi, alisogea hadi mbele ya kizimba kwa woga na huzuni kubwa. Hakimu alimtaka kuieleza mahakama kuhusu maisha yao baada ya mimi kwenda Uganda. Dada yangu alifuta machozi na kusema.

“Ni kweli Paulina ametufanyia mabaya sana na kuharibu kabisa maisha yetu. Mama yangu alipata mshtuko na kupoteza maisha kwa sababu yake. Siku moja alikuja nyumbani na watu na kutuamuru tutoke ndani ya nyumba tuliyokuwa tukiishi akitutishia kutuua, hatukuwa na jinsi kwa kuwa alishakuwa amebadilika sana hakuwa wifi yangu yule mpole.”

Baada ya dada yangu kuongea hayo hakimu alimsogelea na kumuuliza.

“Je, ulitoa taarifa polisi kuhusiana na hilo?”

“Hapana,” dada yangu alijibu.

“Je, una hakika nyumba mliokuwa mnaishi nyinyi ilikuwa ni nyumba ya mdogo wako?”

“Ndio ila hati yake ilikuwa nyumbani kwa mdogo wangu ambako ndiko alilokuwa akiishi na wifi yangu.”

Dada yangu alipojibu hivyo, wakili alimgeukia hakimu na kusema.

“Ndugu hakimu hapa tunahitaji kwanza kupata uhali wa mali alizokuwa nazo marehemu Paulina, kwa kuwa ndizo zinaleta mkanganyiko. Kwa sababu Paulina kuwafukuza hawa katika nyumba yake huenda ni halali kulingana na maamuzi yake endapo nyumba ni yake. Mimi nina ushahidi kuwa mali za marehemu zilikuwa ni zake na si za bwana mshtakiwa Fredy Olutui.”

Aliposema hivyo, aliwataja vijana wa kiume watano, waje kuilezea mahakama, wa kwanza alisema.

“Mimi ninamfahamu bwana Fredy, huyu mtu hakuwa na mali hizi ni mtu masikini, utajiri huu wa ghafla ameupata wapi, wengi tunamfahamu Paulina alikuwa ni mwanamke mchakarikaji.”

Mwingine alisimama na kusema.

“Fredy Olutui miezi mitano iliyopita alikuwa anafanya kazi kwenye kiwanda cha nguo, mimi ni mfanyakazi pale mshahara wake ulikuwa kama wangu shilingi 15,000 leo kuwa na nyumba mbili zenye thamani ya zaidi ya shilingi 100,000 ni jambo la kuchekesha sana.”

Baadaye alikuja mtu aliyekuwa bosi wangu katika kiwanda kile cha nguo na kusema.

“Mara ya mwisho nilimfukuza kazi Fredy kwa kosa la kuiba nguo katika kiwanda changu na kwenda kuuza. Wafanyakazi wengi wa kiwanda changu ni  wa maisha ya kawaida na wote hawana mali kama hizi anazodai ni zake. Wale ninaowalipa mshahara mkubwa nao hawana maisha kama yake amepataje utajiri huu wa ghalfa?”

Maelezo hayo yalizidi kunikandamiza, hakika niliamini kuwa mimi ni wa kufa tu. Haikutosha hapo alikuja shangazi yake na Paulina ambaye alikuja kupigilia kabisa msumari kwa maelezo ya uongo.

“Ni kweli binti yangu Paulina alikuwa mke wa bwana Fredy na alimpenda sana mume wake.  Kutokana na kuwa binti yangu alikuwa ni msichana mrembo miezi miwili iliyopita,  alipata kazi ya kutangaza biashara ya sabuni ya kuogea ya kampuni moja kutoka London ambayo ilimlipa kiasi cha shilingi 300,000. Ushahid huo ni karatasi hizi za mkataba.

Hata hivyo, binti yangu hakuwa na raha kutokana na maisha aliyokuwa akiishi na mumewe. Alikuwa akipokea vitisho kutoka kwa mama yake na mumewe Fredy pamoja na mawifi zake wakimtishia kumuua endapo hata waachia mali zake. Binti yangu aliniambia kuwa alimsikia siku mume wake akipanga mipango yeye na mama yake ya kumuua ili kuchukua mali zake, aliniambia kuwa mumewe alisafiri kwenda Uganda  kwa ajili ya kumtafuta mtu msomi atakayebadilisha mali zake baada tu ya kumuua.”

Nilipoyasikia maelezo hayo ya shangazi yake na Paulina nguvu ziliniishia. Dada yangu na mdogo wangu waliangua kilio wakidai ni maelezo ya uongo.

Mimi sasa niliamini kuwa mipango ya Paulina ya kutaka kuchukua kila kitu changu yalianza muda mrefu na yalipangwa kwa kiwango cha juu sana. Nilishangaa pale shangazi yake alipokuwa akiongea hayo huku akitoa ushahidi wa makaratasi.

Baadaye wakili aliniuliza kuhusu kumuua mwanaume wa Paulina.

“Bwana Fredy, kwanini ulimuua na yule mwanaume aliyekuwa na marehemu Paulina?”

“Nilijue yeye anahusika katika kuharibu maisha yangu,” nilimjibu.

“Ndugu hakimu katika maelezo ya bwana Fredy sikumsikia hata mara moja akimhusisha  bwana Izack na mke wake, kwenye kuporwa mali. Hivyo inaonyesha mshtakiwa aliua ili asiwepo mtu wa kumshtaki endapo atazichukua mali za marehemu. Mimi kama wakili mzoefu kwa maelezo yaliyotolewa na mashahidi, bwana Fredy alitenda makosa kwa dhamira mbaya. Pamoja na hayo hakuna ushahidi wowote kuwa mali zilikuwa zake. Pia ameua watu wawili hivyo kesi ya kuua ni kosa la jinai, ndugu hakimu toa hukumu yako.”

Aliposema hivyo, watu walipiga kelele na kushangilia walioko ndani ya mahakama na nje ya mahakama, kilio kwa dada na mdogo wangu kilizidi.

Hakimu aligonga nyundo yake mara mbili, akajadiliana na mahakimu wake wadogo kisha akatoa hukumu. Alisoma kwenye karatasi na kusema.

“Kutokana na kuridhishwa na maelezo ya pande zote mbili, mahakama imemkuta bwana Fredy Olutui na hatia ya kuua kwa kukusudia, hivyo mahakama inamhukumu adhabu ya kifo.

Nini kitafuatia? Usikose kesho. 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*