NILISHAKUFA

Ilipoishia

Padre aliposema hivyo, askari walinifuta na kunishika, walinipeleka kwenye kitanzi na kunivisha mfuko mweusi. Mmoja alichukua kamba ya kitanzi na kunivisha.

SASA ENDELEA

Nilianza kuhema kwa nguvu, mapigo ya moyo wangu yalinienda haraka zaidi ya siku zote, nilihesabu sekunde tu za kamba kuikaza shingo yangu.

Lakini ghafla nilisikia.

“Achaaaa!!”

Mtu aliongea akiwa mbali na eneo la kunyongea nililokuwepo mimi. Kwa kuwa nilikuwa nimefunikwa mfuko mweusi kichwani, sikujua ni nani aliyekuwa amesema hivyo.

“Mleteni kwa mkuu wa gereza,” aliongea mtu huyo.

Nilibaki na sintofahamu, sikuelewa kabisa nini maana yake na nini kimetokea, kwanini zoezi la kunyongwa kwangu lilikuwa limesitishwa.

Nilishangaa nashushwa kwenye eneo la kitanzi nikiwa nimefunikiwa mfuko mweusi vile vile. Hakika nilizidi kutoelewa, nafsi yangu ilijiuliza mara nyingi sana kwanini napelekwa kwa mkuu wa gereza badala ya kutumikia adhabu yangu.

Nilipelekwa hadi kwa mkuu wa gereza ofisini kwake. Nilikalishwa kwenye kiti.

“Mvueni huo mfuko,” aliongea mtu niliyehisi kuwa alikuwa mbele yangu.

Nilivuliwa mfuko na kukutana na sura ya mtu niliyehisi kuwa nilikuwa namfahamu. Nilibaki namtazama huku na yeye akinitazama. Hata hivyo, nafsi yangu iliendelea kuogopa vile vile ikijua kuwa kifo kilikuwa mahali pale.

Nilipogeuka kushoto na kulia niliwaona watu wanne wakiwa wamevaa mavazi ya kijeshi, aliyekuwa mbele yangu alikuwa na nyota tano begani.

“Fredy bila shaka unanikumbuka?” aliniuliza mwanajeshi huyo.

Nilivuta kumbukumbu yangu iliyokuwa imepotea kutokana na misukosuko ya kuuawa na hatimaye nikamkumbuka vyema. Alikuwa ni yule mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama aliyekuwa mmoja wa viongozi wa Serikali waliotutuma mimi na wenzangu kule Uganda.

“Ndio nakukumbuka,” nilijibu huku macho yakiwa yamenitoka.

“Pole sana Fredy,” aliongea kiongozi huyo kauli iliyoanza kunishangaza.

“Asante nilishapoa kwa sababu naamini mimi ni mtu niliyekufa.”

“Usiseme hivyo Fredy, kuanzia sasa uko huru na utarudi kuendelea na maisha yako,” aliongea kamanda huyo wa jeshi kauli iliyonishtua kupita kiasi.

Nilimtazama macho yakiwa yamenitoka zaidi ya mwanzo, mapigo ya moyo wangu yalianza kukimbia kwa fujo, sikuyaamini maneno yake kwa kuwa hayakuwa huru kwenye masikio yangu.

“Sijakuelewa mkuu,” niliongea mimi huku nikitetemeka.

“Uko huru hutonyongwa,” alirudia tena.

Nilishusha pumzi na kuipandisha, viungo vyangu vilivyokuwa vimepoa kabla ya kukatishwa kwa uhai wangu, viliamka kwa kishindo.

“Pole sana Fredy, wakati unafikishwa mahakamani mimi na wenzangu hatukuwa hapa nchini tulikuwa Tanzania. Tulikwenda kwenye kikao cha kijeshi.”

Aliposema hivyo, aliamuru nifunguliwe kamba za mikono, askari alikuja kunifungulia, hakika nilizidi kushangazwa, nilibaki kama kichaa nisiamani kama naepuka kifo kwa mara nyingine.

Kiongozi huyo wa jeshi aliniuliza.

“Ulitoka vipi Uganda serikali ya Idi Amini haikugundua kazi yenu, maana sisi tulijua tayari mlishauawa.”

“Nashukuru Mungu nilitoka salama,” nilimjibu.

“Wenzako wako wapi?”

“Wote walishakufa,” nilimjibu huku tone la chozi likinidondoka.

Nilimsimulia kila kitu kilichponipata Uganda, jinsi nilivyonusurika kifo zaidi ya mara moja. Wakati namsimulia, machozi mengi yalikuwa yakinitoka maana nilimsimulia kwa hisia nzito.

Baadaye pia nilimsimulia jinsi Paulina alivyoharibu maisha ya familia yangu, hadi ikapelekea kumuua. Kiongozi huyo aliniambia pia jambo lilonishangaza.

“Sisi Serikali ambao tulikutuma Uganda, tulijua kuwa mkeo hawezi kuyathamini maisha yako, ingawa tulimruhusu awe anachukua pesa zako benki, lakini tulikuwa tukimchunguza mwenendo wake. Tulijua kuwa mwanamke yule si mtu mzuri hivyo tulimpeleleza sana na kujua kila kitu chake. Nadhani kosa ambalo wewe ulitakiwa uhukumiwe ni kujichukulia sheria mkononi na si vinginevyo, kwa kuwa yule mwanamke alikuwa anastahili kuuawa. Sisi kama serikali tutahikikisha tunamshtaki yule mwanamke hata kama kwa sasa yuko kaburini.”

Maneno ya kiongozi huyo wa jeshi yaliniacha mdomo wazi, sikuamini nilihisi ni ndoto.

“Fredy wewe ni mtu muhimu sana kwenye nchi hii, umefanya kazi kubwa Uganda. Hivi sasa kambi ya jeshi aliyokuwa amepanga kuingamiza Idi Amini hawezi tena kuingamiza, kwani tumejipanga kabla hajatuma makomandoo wake. Na tulikwenda Tanzania kuomba msaada kwao wa kuweza kufanikisha kuwazunguka kabla hawajaikanyaga ardhi ya Kaisavuna.”

“Asante sana mkuu ni ngumu kuamini, nashukuru kwa kulipa fadhila zangu,” niliongea mimi nikitokwa na machozi.

Baada ya maongezi hayo, niliachiwa huru, kiongozi huyo wa jeshi aliamuru nilindwe hadi hotelini. Nikiwa ndani ya gari aina ya Land Rover niligeuka kulitazama gereza, machozi mengi yalinibubujika.

Nilipelekwa hoteli moja ya hadhi ya juu iliyokuwa pembeni ya Wilaya ya Kuasheni. Viongozi hao waliniambia kuwa nikae hadi pale akili yangu itakapotulia na pindi Serikali itakapokuwa  ikimshtaki Paulina mahakamani.

Usiku nikiwa chumbani, nilipiga goti na kulia usiku kucha, nilimlilia Mungu nikiomba anisamehe dhambi zangu. Nilimuuliza Mungu mimi nilikuwa ni nani kwanini alikuwa ameniepusha na kifo zaidi ya mara nne. Nilimshukuru mara nyingi isivyoweza kuhesabika, nikilia kama mtoto mdogo.

Baada ya siku mbili, nikiwa bado hotelini, nilisikia habari kwenye redio ya Kaisavuna kuwa serikali imemshtaki Paulina Luta kwa kosa la kumuua mtu aliyefahamika kwa jina la Kaselo Tuendo aliyekuwa mmiliki wa klabu ya Freesize.

Kumbe Paulina alishirikiana na mke wa bwana huyo kumuua ili ainunue klabu hiyo kutoka kwa mkewe. Yaani mke wa Kaselo na Paulina walimuua Kaselo ili Paulina ainunue klabu hiyo, kwa kuwa bwana huyo alikataa kuuza klabu hiyo.

Pia Serikali ilimshtaki Paulina kwa makosa mengi yakiwemo ya usambazaji wa mihadarati. Raia wa Kaisavuna walianza kuilalamikia mahakama kwa kunihukumu mimi kunyongwa. Wengi walisema kuwa kwa makosa hayo Paulina alikuwa anastahili kuuawa.

Pia ilimshtaki yeye na watu kadhaa kwa kuharibu maisha yangu, hata hivyo raia wengi walijua kuwa tayari mimi nilishakuwa nimenyongwa.

Mawakili wa serikali waliihoji mahakama kupitia ibara ya sita ya kipengele cha katiba ya Kaisavuna kuwa, kama Paulina aliyafanya hayo basi mimi ilitakiwa niwe huru hata kama nilijichukulia sheria mkononi.

Serikali pia ilimshtaki shangazi yake na Paulina kwa kushirikiana na binti yake katika uhalifu. Mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 12 jela.

Kesho yake nilitoka hotelini na kuelekea nyumbani kwa Halid. Niliwakuta dada na mdogo wangu pamoja na baadhi ya ndugu na majirani wakiwa wamekusanyika. Ilionyesha walikuwa  wakihani msiba wangu.

Niliposimama mlangoni Salah hakuamini alihisi ni ndoto. Alinirukia na kunikumbatia, alinibusu mara nyingi huku akilia sana.

Mdogo wangu Zuni aliponiona, alipigwa na butwaa, alimuita dada aliyekuwa ameketi kwenye mkeka kwa huzuni, dada aliponiona alisema.

“Huu ni muujiza.”

Alinikimbilia na kunikumbatia. Wote tulilia sana huku majirani nao wakipigwa na butwaa. Mke wa Halid pamoja na watoto wake nao walikuja kunishangaa. Hakika lilikuwa ni tukio la ajabu sana kwenye maisha yao. Nilimfuata Halid aliyekuwa hajiwezi kitandani na kumkumbatia na kulia mbele zake.

Siku ya pili yake mimi na watu wote tulishangaa kusikia hotuba ya Rais wa nchi yetu akinitaja mimi. Alisema kuwa anaiomba mahakama imuachie huru Fredy Olutui.

Jambo zuri zaidi mahakama iliamuru kuwa mali zote za marehemu Paulina zirudishwe kwenye mikono yangu. nyumba tatu za kifahari, magari mawili, na maduka sita ya nguo.

Sikuamini siku nilipokabidhiwa hati za mali hizo, mdogo wangu nilimrudisha shuleni, furaha ya familia yangu ilirudi.

Nilikwenda kujengea kaburi la mama yangu, nilimuomba msamaha mara nyingi nikidondosha machozi juu ya kaburi lake. Baada ya wiki moja nilimsafarisha rafiki yangu Halid kwenda kutibiwa nje ya nchi. Nilimpeleka London ambako alifanyiwa matibabu kwa muda wa miezi mitatu.

Siku nikiwa nimepumzika nyumbani kwangu, mlango wa sebuleni uligongwa, nilipokwenda kufungua, nilikumkuta Salah akiwa amesimama akiwa na tabasamu la kutosha. Kutokana na pesa nyingi nilizokuwa nimempa, alikuwa amekwenda kununua nguo na vitu vingine vya urembo.

Hakika nilibaki nimeduwaa kwa njisi alivyokuwa amependeza, alikuwa ni msichana mzuri zaidi ya nilivyomjua.

Upesi tulikumbatiana, nami nilivaa  vizuri tukaondoka nyumbani kuelekea sehemu moja ya mapumziko, huko nilimvalisha pete ya uchumba. Baada ya mwezi Halid akiwa amerudi akiwa na afya njema viungo vyake vikiwa vimeimarika, mimi na Salah tulifunga ndoa kanisani. Hakika sikuamini kama nimemuoa Salah msichana aliyekuwa amenionyesha maajabu ya mapenzi na nini maana ya msemo usemao, mke mwema anatoka kwa Mungu.

Baadaye niliamua kumtumikia Mungu kwa kutembea ndani na nje ya nchi kulihubiri neno lake, nikitoa ushuhuda wa maisha yangu uliowaacha wengi midomo wazi na kuwashtua.

Kiukweli namshukuru Mungu amenionyesha kuwa yeye anaonekana wakati wote sio kwa macho, bali kwa matendo yake ya ajabu yanye kuogopesha, asanteni kwa kunisikiliza. Naitwa Fredy Olutui.

MWISHO

Kama hukusoma hadithi hii tokea mwanzo, Like page yangu ya Facebook, inayoitwa Hadithi za Eman Fisima ili uweze kuisoma yote. Asante kwa kuwa nami, Mungu akubariki.

Previous Article
Next Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*