NILISHAKUFA-26

NA EMAN FISIMA

Ilipoishia

Sikutaka kumwambia kuwa mama yangu alikuwa amenikataza kwenda Uganda. Usiku huo alianza kunishika kila sehemu ya mwili wangu. Mahaba mazito yalinivamia, nilijihisi niko kwenye paradiso ya anga.

SASA ENDELEA

Sio siri Paulina alikuwa ni mwanamke mwenye kila aina ya ujuzi acha ule wa kujua kupika, kujua kubembeleza na vingine vingi, Paulina aliyaweza mambo yote.

Kazi yake ya kitandani, ilinichanganya sana mimi Fredy. Hiyo ndiyo iliyokuwa ikiniongezea uchizi na kunifanya nimwone Paulina kama malaika. Ilinifanya niamini kuwa wanaume wenzangu hawapati raha kama  ninayoipata mimi.

Usiku huo Paulina alinifanyia utundu wa kila aina. Hakika moyo wangu ulikataa kabisa kumwacha. Nguvu ya kwenda Uganda iliongezeka maradufu. Maana niliamini maisha mazuri na pesa ndivyo vitakavyoendelea kunipa raha kama zile na kuisimamisha vema ndoa yangu.

Shughuli hiyo ilifanyika nusu nzima ya usiku. Asubuhi niliamka nikiwa nimechoka sana, maana mchakamchaka niliopelekeshwa jana usiku, ulikuwa si kawaida.

Paulina aliniandalia maji ya kuoga na kuniogesha yeye mwenyewe. Lile tabasamu lake zuri lilirudi kwa mara nyingine, safari hii nikiliona ni zuri zaidi ya lile la kwanza. Hakika alizidi kunivutia sana mwanamke huyu.

“Asante sana mke wangu naona bahati kuwa na mke kama wewe,” niliongea mimi wakati nikifutwa maji kwa taulo jeupe.

“Usijali wewe ni mume wangu. Unastahili kila kitu kutoka kwangu,” aliongea Paulina kwa sauti iliyozidi kunilevya.

“Nitakukumbuka sana pindi nitakapokuwa Uganda. Nitaomba uniandikie barua hata mara moja nami nitafanya hivyo.”

“Usijali nitafanya hivyo. Ila mwezi mmoja ni mkubwa sana mume wangu. Nitaishi kwa tabu sana kwani nimeshakuzoea.”

“Lakini Paulina mke wangu si ulikuwa unataka kunikimbia kwenda kwenu wewe?” Nilimuuliza kwa tabasamu huku nikimshika kidevu.

Alijichekesha na kunijibu.

“Ni hasira tu mume wangu. Unajua sijazoea kuishi maisha ya shida. Toka nikiwa mdogo nimelelewa katika maisha ya raha yasiyo na shida yoyote. Hivyo naomba unisamehe.”

“Usijali hata hivyo ulinifanya niongeze bidii ya kutafuta kazi.”

“Kweli mume wangu?”

“Kweli kabisa mke wangu.”

Furaha ya Paulina ndiyo ilikuwa furaha yangu. Hakuniita tena Fredy kama miezi kadhaa iliyopita, bali aliniita mume wangu.

Siku hiyo nilimuaga na kuondoka nyumbani. Nilielekea moja kwa moja kwenye lile jengo la Serikali, jengo ambalo nilipatia kazi ya kwenda Uganda.

Tayari akili yangu ilishakuwa imesahau kuwa mama yangu mzazi alikuwa amenikataza kukubali kazi hiyo. Sikulikumbuka zuio la mama la mimi kwenda Uganda kwa Idi Amini.

Sikujiona ni mwenye kiburi na mkaidi, bali nilichotaka mimi ni kuhakikisha naendelea kula raha na mke wangu Paulina, huku mama na dada zangu, wakiishi maisha mazuri. Niliamini safari yangu ya Uganda itanifanya nipige  ndege watatu kwa jiwe moja.

Ndani ya chumba cha jengo hilo la Serikali, niliwakuta wale wenzangu sita ambao nitaondoka nao kwenda Uganda. Huko tulifundishwa mambo mengi likiwemo jambo zito la kushika silaha.

Nilikuwa mwoga sana wa kushika bastola, maana katika maisha yangu sikuwahi kufikiria kama siku moja nitakuja kushika bunduki au silaha yoyote ya kijeshi. Kwa kiasi kidogo nilikuwa mwoga. Tabasamu la mrembo, mke wangu Paulina, ndilo lililonipa kujiamini.

Tulifundishwa mengi sana. Kiongozi wa jeshi la ulinzi la Kaisavuna alisema tutagawana majukumu.

“Tayari tuna mtu wetu wa kutoka hapa   ambaye yuko kule. Yeye anafanya kazi kwenye kitengo cha ajira cha jeshi la Uganda. Mkifika atawapa vitambulisho vya kijeshi na nguo. Kwa hiyo mtakuwa kama wanajeshi wa jeshi la Uganda. Yeye mwenyewe atawapa majukumu ya kujiunga na ulinzi wa sehemu mbalimbali kwenye vitengo vya Serikali,” aliongea kiongozi huyo.

“Lakini angalizo kuu tunaomba mjitahidi, kujivika uraia wa Uganda. Uzuri ni kwamba lugha ya Kaisavuna na Uganda ni moja ila mjitahidi kukirekebisha Kiswahili chenu kifanane na cha Uganda. Katika lugha hizi mbili mjitahidi kuongea kama Waganda,” aliongeza kiongozi mwingine wa Serikali.

Tuliendelea kuelekezwa mambo mengi sana kuhusu kazi hiyo ngumu tutakayoifanya tukiwa ndani ya Uganda.

“Tukiwa Uganda tuwasiliane vipi na familia zetu. Maana barua zinachelewa kufika?” niliuliza mimi.

“Ili kuonyesha tunawajali  nyinyi wenyewe mtawachagua ndugu zenu au wake zenu watakaokuwa wanakuja kuongea na nyinyi hapa kwa njia ya simu au kupata taarifa zenu kutoka kwetu,” alijibu kiongozi yule wa jeshi.

Taarifa hiyo ilinipa faraja, niliamini kuwa Serikali ilitutuma Uganda kwa lengo zuri la kuilinda nchi yetu kivita dhidi ya Idi Amini. Nilifurahi kuona ndugu zetu au wake zetu watakuwa wanakuja pale kwa ajili ya kuongea na sisi kwa njia ya simu.

Tuliendelea kupewa mafunzo hayo kwa siku nyingine tatu. Siku ya nne kila mmoja alipewa kiasi cha shilingi 60,000  pesa iliyokuwa nyingi ambayo hatukuwahi kuishika tokea tuzaliwe. Mimi nilichanganyikiwa kuona pesa ile mikononi mwangu.

“Tunaomba pesa hiyo ikamalize baadhi ya matatizo yenu nyumbani. 60,000 nyingine tutawapa mkiwa mnaondoka kwenda Uganda,” aliongea mwanamke mmoja wa ndani ya Serikali.

Siku hiyo nilirudi nyumbani na kumpa mke wangu Paulina shilingi 15,000. Sikutaka kumwambia kuwa nilikuwa nimepewa 60,000, kwani nilitaka niifanyie mambo mengine pasipo yeye kujua. Hakika alifurahi sana mimi kumpa 15,000. Sasa aliamini maisha yake yatarudi na kuwa mazuri zaidi alinikumbatia na kunibusu mara nyingi.

Siku iliyofuata, nilitoa kiasi cha shilingi 30,000 na kununua nyumba nyingine. Nyumba iliyokuwa nzuri yenye kuendana na urembo wa mke wangu. kisha shilingi 7,000 niliikarabati ile nyumba niliyokuwa nikiisha na Paulina, nikihitaji mama na dada zangu waje kuishi pale.

Nilitumia njia ya uongo kumwambia mama kuhusu mimi kupata pesa ya kujenga nyumba ile. Nilimwambia kuwa pesa ile nilikuwa nimepata kutoka katika mkopo wa jumuiya ya watu wa Uingereza, waliokuja nchini kuwakomboa vijana, huku nikimwambia uongo mwingine kuwa pesa nyingine nitakayopewa, nitafungua biashara.

Mama yangu alifurahi sana, alimshukuru sana Mungu kwa neema hiyo ya ghafla. Tukiwa tumekaa nyumbani baada ya  kuwahamishia tulikokuwa tunaishi mimi na kipenzi changu Paulina, mama aliniuliza swali lililoniumiza kisiri.

“Mwanangu si unakumbuka nilikwambia kuwa achana na safari ya kwenda Uganda, Mungu atakuletea neema nyingine?”

“Ndio mama nakumbuka,” nilimjibu kwa tabasamu la uongo huku moyo wangu ukitetemeka.

“Unaona sasa umepata bahati hiyo. Sasa naomba ujitahidi kufanya biashara, hii ndiyo bahati, haitajirudia tena. Fanya kazi kwa bidii, itendee haki hela uliopewa,” aliongea mama yangu maneno yaliyonifanya nikose amani.

Kwa mara ya kwanza nilikuwa nimemdanganya mama yangu. Sikuwa na jinsi nilimwomba Mungu anisamehe kimoyo moyo. Nilimdanganya pia kuwa nasafiri kwenda jimbo la Baikakulu kwenda kufuata biashara.

Siku inayofuata nilikwenda kwa rafiki yangu Halid na kumsimulia kila kitu. Sikutaka kumficha kuhusu safari yangu ya Uganda. Maana yeye ndiye mtu wangu wa karibu, atakayenisaidia kuiangalia familia yangu pindi nitakapokuwa nimeondoka.

Hakupendezwa na uongo wangu jinsi nilivyomdanganya mama yangu. Lakini nilimsihi akubali uamuzi wangu kwani sikupenda nife masikini mimi na familia yangu. Pia nilimwambia kuwa, bila kufanya hivyo, Paulina atanikimbia na kurudi kwao kwani maisha ya tabu hakuwa ameyazoea.

Halid alinielewa japo kwa tabu, baadaye aliniahidi kuwa atakuwa anakwenda kuitazama familia yangu pamoja na mke wangu.

Siku ya Jumapili nilikaa mimi na familia yote nyumbani kwangu. Tulipika chakula kizuri. Mama yangu, dada yangu na mdogo wangu Zuni walijua kuwa nakwenda Baikakulu. Aliyekuwa akijua  kuwa nakwenda Uganda alikuwa ni mke wangu Paulina.

Mama yangu alizidi kupendezwa na tabia nzuri ya Paulina, hata mimi nilifurahia kuona mke wangu akiijali familia yangu kiasi kile. Kila mmoja alimpenda Paulina hata watoto wadogo wa dada yangu. Siku hiyo ilikuwa ni furaha ndani ya nyumba yangu.

Nilifarijika pale Paulina aliponiambia kuwa anaomba familia yangu wakae pale kwa siku tatu kwani alikuwa amewakumbuka sana. Sikuwa na kipingamizi nilipendezwa sana na ukarimu wa mke wangu.

Siku ya Jumanne tulikutana tena mimi na wale wenzangu sita katika lile jengo la Serikali ambapo tulipewa mafunzo mengine na maelekezo ya kutosha kuhusu kazi yetu ya upelelezi nchini Uganda.

Baadaye tulipewa kiasi kingine cha pesa shilingi 60,000. Pesa itakayotusaidia kumalizia matatizo ya nyumbani kwetu. Nilizidi kuwa na furaha hata woga ule wa kwenda kwenye nchi isiyo na amani, ulikuwa umepotea.

Nini kitafuatia? Usikose kesho.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*