Niacheni: Koscielny agoma kurudi, alazimisha kupigwa bei Arsenal

LONDON, England

HALI si shwari katika kikosi cha Arsenal, wakati huu ambao mashabiki wao wametulia wakisubiri kuona timu yao watasajili mchezaji gani, mambo yamezidi kwenda mrama.

Mpaka sasa wamefanikiwa kupata saini ya mchezaji kinda kutoka Brazil, wala mashabiki wa Arsenal hawajashtuka, jambo pekee ambalo linawatia hofu ni hili la nahodha wa kikosi hicho, Laurent Koscielny kugoma kurudi akishinikiza kuuzwa.  

Katika hali ya kushangaza ni kwamba beki tegemeo wa Arsernal, Koscielny, amempa wakati mgumu kocha wa timu hiyo Unai Emery, baada ya kugoma kusafiri nchini Marekani, ikiwa ni ziara ya kujiandaa na msimu mpya.

Imedaiwa Koscielny anatumia nguvu kuushawishi uongozi wa klabu hiyo kumpiga bei katika dirisha hili la usajili baada ya kuitumikia kwa muda miaka nane.

Na hiyo ni kutokana na kwamba Arsenal wapo mbioni kumsajili beki mpya William Saliba, akitokea St Etienne kwa ada ya uhamisho milioni 27 (sh bil.61) hata hivyo ataendelea kubaki katika klabu yake hiyo kwa mkopo wa msimu mzima.

Arsenal methibitisha kitendo cha beki huyo raia wa Ufaransa kugoma kusafiri na kikosi kizima cha Arsenal.

“Tumesikitika sana kwa kitendo hicho ambacho ni kinyume na sheria zatu, naamini ishu hii itatatuliwa na kutoa tamko rasmi,”

Aidha klabu ya Bordeaux, inamnyemelea kwa ukaribu Koscielny, huku timu zingine zikiwamo Lyon na Rennes zikimfukuzia ili kumnasa.

Koscielny, mwenye umri wa miaka 33, amejiunga na Arsenal mwaka 2010 akitokea Lorient, akiwa na Washika Bunduki hao wa London, amefanikiwa kubeba mataji mawili ya Kombe la FA.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*