googleAds

NI WAKATI WA KUANZISHA MASHINDANO YA KUDANSI KITAIFA 2O17

HERI ya Mwaka Mpya msomaji wangu mpenzi, naamini umeuona mwaka kwa uzuri na kwa matumaini mapya juu ya malengo uliyojiwekea. Tumekutana tena leo kwenye makala haya kujadili masuala ya sanaa ya kudansi na ile ya maonesho kwa ujumla.

Leo nataka niwakumbushe wadau wote wa sanaa hii ya kudansi kwamba kuna sehemu tumekosea. Labda niwape kumbukizi kidogo ili wasomaji wangu muweze kunipata vizuri. Miaka ya 1980 kulikuwa na mashindano ya kudansi, wakati ule wakina Tasi Chiume, Elvis Cool, Chuche na wengine yalikuwa mashindano ya utashi tu wa club husika kama vile Msasani Club, YMCA, RSVP pale Mbowe.

Hayo yalikuwa mashindano yasiyo rasmi kama nilivyosema japokuwa yalikuwa mazuri na yenye msisimko sana. Nimegusa kidogo tu kipindi hicho ili nikulete kwenye mada kuu ya leo.

Mashindano mengine yalikuwa miaka ya kuanzia 1988, bingwa alikuwa Digadiga, pia ilifanyika mashindano mwaka huohuo pale Motel Villa (Moon Dust) Mwananyamala, mashindano haya yalikuwa ya wawili wawili tulikuwa tunayaita Storms. Nataka Niwaambie haya mashindano yote yalikuwa yanafanywa au kuendeshwa na watu wazima waliokuwa wameenda shule ila walijua thamani ya sanaa ya kudansi.

Ngoja niwakumbushe jambo ambalo limenisukuma kuandika makala ya leo, mwaka 1984 yalifanyika mashindano ya kwanza kabisa pale Mbowe Hotel (RSVP), wakati ule mitindo ya uchezaji ulikuwa Robot na Break dance ndio inaingia, mdhamini wa mashindano hayo alikuwa kampuni moja ya ndege, ilikuwa inaitwa ASAS Airline.

Wachache wa washiriki walikuwa Omari (Ommy Sydney) Mzee Bachu, Eddy, Chuche, Nico Scaba Scuba, Digadiga, wanawake kulikuwa na Tanisa, Lukia na wengine. Hiyo ilikuwa Mbowe, mwaka huo huo yalifanyika mashindano YMCA City Centre Agosti na washiriki waliongezeka nitaielezea hii makala nyingine, baada ya hapo 1989 ndipo yalipoanzishwa mashindano ya Taifa, yalianzia Motel Villa baadaye yakapelekwa pale DI (Dar es Salaam Institute) hapo bingwa wa taifa anaibuliwa, ambaye alikuwa Black Moses, wa pili Ommy Sydney na wa tatu Digadiga.

Mwaka 1990 mashindano ya taifa yalifanyika Lang’ata Kinondoni pale mshindi wa kwanza alikuwa Ommy Sydney, wa pili Black Moses, wa tatu Masha Ismail ambaye alikuwa mtoto wa marehemu Sheikh Yahya Husein, huyu mtabiri maarufu na mnajimu Afrika Mashariki.

Nitayataja mashindano mengine makala ijayo na nitakutajia majaji na wageni wa heshima ili ushangae vipi leo hatuthamini hiki kitu, wito wangu kwa wadau wote wa sanaa hii ya kucheza muziki wakutane ili turudishe msisimko ule, vipi tunaacha kitu ambacho kilikuwa kinawakutanisha vijana kutoka sehemu mbalimbali Tanzania halafu wakatoa burudani na kufundisha mitindo mbalimbali ya kudansi na kutoa ajira?

Isitoshe kuna vitu vingi vinajitokeza pale kama kuonana na viongozi wa ngazi mbalimbali, wakurugenzi wa makampuni makubwa (fursa). Tukiyarudisha haya mashindano baada ya muda mfupi tutashangaa tunatengeneza ajira pana ndani na nje ya nchi, inawezekana naongea jambo ambalo watu wengi watashangaa, lakini kuna baadhi ya nchi hapa Afrika vijana wengi wako nchi za nje kwa kupitia fani ya kudansi tu na sasa ni wawekezaji kwenye nchi zao.

Hivyo mwaka huu 2017 ni muhimu sana wadau kukaa chini na kutafakari upya namna ya kuyafufua mashindano ya dansi ya Taifa, vijana wapo tena wenye uwezo mkubwa na wapo katika kila mmoja ni vyema wadau tukajipanga kuhakikisha mashindano haya yanarejea mwaka huu ili kuipa thamani fani ya kudansi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*