Ni kweli Coutinho mguu nje mguu ndani Barca

MADRID, Hispania

 STAA Philippe Coutinho, amekiri akisema kwamba ni kweli siku zake zinayoyoma katika klabu ya Barcelona, baada ya usiku wa kuamkia jana kuifungia bao timu yake katika ushindi wake wa mabao 5-1 dhidi ya Lyon  katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora.

Coutinho ndiye aliyefunga bao la pili, baada ya straika, Lionel Messi, kufunga la kuongoza katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Camp Nou na kuifanya Barca kutinga hatua ya robo fainali, baada ya timu hizo kushindwa kufungana katika mchezo wa kwanza wakiwa ugenini uliopigwa mwezi uliopita.

Nyota huyo wa timu ya Taifa ya Brazil, alipachika bao akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Arthur na staa mwenzake wa zamani Liverpool,  Luis Suarez na kisha  Messi akaongeza jingine na mengine mawili kutoka kwa  Gerard Pique na staa aliyetokea benchi, Ousmane Dembele, yakawahakikishia ushindi huo.

 Tangu asajiliwe kwa ada ya Euro milioni 142 Januari mwaka jana akitokea Liverpool, Coutinho, ameshindwa kuwa kwenye ubora wake jambo ambalo limeshazua tetesi kuwa anataka kurejea katika michuano ya Ligi Kuu England.

Juzi nyota huyo alikiri kiwango chake kuwa chini na matarajio yao na hakuweza kukataa kama anataka kuondoka katika timu hiyo mabingwa wa  La Liga.

 “Katika kipindi cha wiki chache zilizopita ama miezi kadhaa sikuweza kucheza vizuri, lakini bado nataka kuimarika,” alisema Coutinho, katika mahojiano na magazeti ya The Mirror na  Metro.

“Nilikuja Barcelona kutoa mchango wangu. Ninaishi kwa kumbukumbu. Huwezi kufahamu ni kitu gani kipo mbeleni, lakini kwa leo (juzi) nimefurahishwa na kiwango changu,” aliongeza staa huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*