Ngassa, Dante wanazidi kutufumbua macho juu ya tatizo la soka letu

NA MOSES FRANCIS

NILIKUWA nalifuatilia pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga ya Dar es Salaam dhidi ya Prisons ya jijini Mbeya lililochezwa Jumatatu ya wiki hii lililopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Ni pambano ambalo limeniacha na maswali mengi ya kujiuliza bila ya majibu kwani lilitawaliwa na fujo pamoja na vurugu ambazo zilikuwa zinazuilika. Ndio, wachezaji wote wa timu mbili walikuwa na uwezo wa kulimaliza pambano hilo salama salimini bila ya kurushiana ngumi au kupigana vichwa.

Wachezaji ambao walidhani wanaonewa katika mechi hiyo, walikuwa wana uwezo wa kuzistahimili hasira zao vifuani na baadaye wakacheza mpira. Sikatai, mchezo wa soka kuna wakati wachezaji huwa wanapatwa na hasira, lakini kama mchezaji wa kulipwa au mchezaji yeyote yule, hupaswi kurusha ngumi kwa refa au mchezaji wa timu pinzani ili umalize hasira zako. Daima haipo hiyo duniani.

Katika mechi hiyo, tatizo lilianzia kwa beki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’, ambaye alionyesha nia ya kumpiga kichwa mwamuzi wa mchezo huo, baada ya kutoa penalti kwa Prisons.

Dante na wachezaji wenzake wa Yanga walikuwa wanadai ilikuwa si penalti halali. Mashabiki wao nao waliokuwepo uwanjani wakasimama wakawa wameungana na mawazo ya wachezaji wao kuwa penalti ile iliyotolewa na mwamuzi ilikuwa si halali.

Lakini hapo hapo, ukiachana na suala la uhalali au kutokuwa halali kwa penalti ile, Yanga walikuwa wameutawala mchezo huo. Walikuwa na uwezo wa kukubaliana na uamuzi wa refa na baadaye wakaendelea kucheza soka kwa ajili ya kusawazisha bao lile kama ambavyo walivyokuja kufanya kipindi cha pili.

Walikuwa wana dakika nyingine 45 za kukomboa bao lile na baadaye kutafuta bao la ushindi bila ya kuanzisha fujo yoyote.

Tukio jingine lilikuwa ni la Mrisho Ngassa. Yeye akiwa hana mpira, aliruka juu na kumpiga kichwa mchezaji wa Prisons, Hassan Kapalata. Ni tukio la aina yake katika mchezo wa soka na ni tukio ambalo halipaswi kuchekewa.

Lakini katika nchi yetu hii, matukio ya namna hii mara nyingi yamekuwa yakijirudia mara kwa mara. Ni matukio ambayo kwa jinsi siku zinavyozidi kwenda, yanaonekana kuzoeleka na yanaonekani ni matukio ya kawaida katika mboni ya macho yetu.

Kuna tatizo kubwa mahala fulani. Mshambuaji wa Simba, John Bocco pamoja na beki wa kati wa Kagera Sugar, Juma Nyoso, nao wamewahi kukutwa na hatia ya makosa ya aina hii.

Ni makosa ambayo yaliwaweka nje ya uwanja kwa muda fulani. Pamoja na adhabu zilizotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwenda kwa wachezaji hawa, lakini kuna wachezaji bado wamekuwa hawataki kubadilika.

Hapa ndipo ninapoendelea kuamini kuwa katika nchi hii, kuna wachezaji wachache sana ambao wanajitambua.

Kwa hiyo, kwa haya matukio ya aibu yaliyofanywa na kina Ngassa pamoja na mwenzake Dante, yanatoa picha halisi ya soka letu. Tunaishi katika nchi ambayo klabu zetu za soka huwa hazina utaratibu wa kuadhibu wachezaji wao pindi wanapofanya makosa ndani na nje ya uwanja.

Kwa mtindo huu, ni vigumu tabia kama hizi za utovu wa nidhamu ndani ya uwanja kukoma. Na matokeo yake, timu za klabu zetu na hata ya Taifa, Taifa Stars, zitaendelea kuwa wasindikizaji katika michuano mbalimbali ya kimataifa.

Ndio maana wakati mwingine nashindwa kumtupia lawama Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, kwa kile kilichotokea Lesotho wakati timu yetu ilipocheza na timu ya taifa ya nchi hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*