googleAds

Ngassa anukia unahodha Yanga

MICHAEL MAURUS

BAADA ya Ibrahim Ajib kuondoka Yanga, kitambaa cha unahodha ndani ya timu hiyo kwa sasa kipo wazi kwa wachezaji watatu, miongoni mwao, akiwa ni winga machachari, Mrisho Ngassa.

Ajib aliyetimkia Simba baada ya mkataba wake Jangwani kumalizika, alipewa cheo hicho kutoka kwa Kelvin Yondani, huku msaidizi wake, akiwa ni Juma Abdul.

Lakini wakati nafasi kubwa ya unahodha ikionekana kuwa wazi kwa Yondani, kuna kila dalili ya beki huyo wa kati mpambanaji hasa, kukisoka cheo hicho.

Hilo linatokana na ukweli kuwa hadi sasa Yondani hajaonekana mazoezini kwa sababu nambazo bado zimeendelea kuwa gizani, huku Ngassa akibaki kuwa mkongwe ndani ya kikosi hicho kinachojifua kwenye Uwanja wa Chuo cha Biblia, mjini hapa.

Mbali ya ukongwe wake, Ngassa ana sifa za uongozi kutokana na kuifahamu vilivyo Yanga, akiwa ni miongoni mwa wachezaji waliowahi kutamba na kupendwa mno na mashabiki hadi viongozi.

Mbali ya Ngassa, mwingine mwenye uwezo wa kupewa unahodha ni kiungo Pappy Tashishimbi ambaye hata hivyo, japo ni mgeni haufahamu vilivyo utamaduni wa Yanga kama ilivyo kwa winga huyo, maarufu kwa jina la Uncle.

Japo benchi la ufundi la Yanga limekuwa kimya juu ya suala zima la cheo cha unahodha baada ya kuondoka kwa Ajib, lakini kuna tetesi kuwa kitendo cha Yondani kutoonekana mazoezini hadi sasa, kitamfanya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera kumpa jukumu hilo mchezaji mwingine.

“Nadhani unafahamu msimamo wa Zahera katika suala zima la nidhamu, akijua Yondani hayupo mazoezini hata kama ana sababu za msingi, hawezi kumpa unahodha, atamfikiria mwingine. Anaweza kuwa Tshishimbi au hata huyo Ngassa,” alisema mmoja wa watu wa ndani ya Yanga.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*