NEVILLE ATAJA WABAYA WAKE

MANCHESTER, England

BEKI wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, hivi karibuni alibainisha wachezaji ambao walimpa wakati mgumu alipokuwa uwanjani na anaowakubali.

Neville aliyekuwa anakipiga nafasi ya beki wa kulia katika kikosi cha Manchester United, alibainisha hayo kwenye mtandao wake wa kijamii wa twitter aliporuhusu mashabiki wake kumuuliza maswali.

Shabiki mmoja aliyejulikana kwa jina la Jay Patton, alimuuliza kuwa ni straika gani ambaye aliwahi kumsumbua wakati anacheza na hataweza kumsahau, lakini mwingine alimuuliza beki gani aliyefahamika kwa jina la Triggz, aliuliza ni beki gani bora aliyewahi kucheza dhidi yake.

“Romario ni mshambuliaji hatari zaidi ambaye nimecheza dhidi yake, ana kasi kubwa, akili ya kutambua pia uwezo wa kupiga chenga.

“Alinisumbua na kuniogopesha sana wakati alipokuwa anakuja kwa kasi upande wangu, siwezi kumsahau,” alisema Neville ambaye ni mmoja wa wachambuzi wa kituo cha Sky Sports.

Pia, alimtaja beki mkongwe wa AC Milan, Paolo Maldini, kuwa ndiye bora kuwahi kucheza dhidi yake kipindi hicho walipokutana katika Ligi ya Mabingwa na hata timu za Taifa Italia na England.

“Maldini alikuwa bora sana kwa beki wote ambao nimewahi kukutana nao kwa kipindi chote nilichokuwa uwanjani.

“Ana nguvu na uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo hakika alikuwa bora kwa kipindi chote,” alisema Neville aliyetwaa mataji mengi akiwa Manchester United.

Previous Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*