googleAds

Ndayiragije apewa ukocha Taifa Stars

NA WINFRIDA MTOI

KUTOKANA na mashabiki kutamani kocha wa muda wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, apewe majukumu ya kuwa kocha mkuu rasmi wa kikosi hicho, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limefunguka na kusema anastahili.

Baada ya kufanikiwa kusonga mbele hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia 2022 kwa ukanda wa Afrika kwa kuitoa Burundi, mashabiki wamekuwa na maoni tofauti wakitaka aendelee na majukumu hayo.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo, alisema wanachokisema ni sahihi kwasababu Ndayiragije ana sifa zote za kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars.

Alisema hata alivyopewa majukumu hayo kwa muda, alionekana ana sifa hiyo ya kufundisha timu ya taifa, lakini kwasasa watu wanatakiwa kusubiri uamuzi utakaotolewa kulingana na taratibu za kiofisi.

“Hadi kupewa majukumu ya sasa ina maana anafaa, kama tungekuwa na wasiwasi naye, asingekuwa kocha wa muda, tusubiri uamuzi utafanyika siku si nyingi kila mmoja atajua,” alisema Mirambo.

Kwa upande wa Azam FC, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin maarufu Popat alisema, hakuna shida kwa kocha wao kupewa majukumu ya timu ya taifa na watampa baraka zote, endapo suala hilo litatokea kwasababu wanafahamu uwezo wake wa kufanya kazi sehemu zote mbili.

“Kocha wetu akiwa moja kwa moja timu ya taifa, sisi hatuna tatizo, tunamuamini anafanya kazi yake kwa weledi, ukiangalia tangu amepewa majukumu hayo kwa muda, bado amekuwa akiendelea na program yake hapa Azam FC.

“Ukweli uliyopo huyu kocha anajua jinsi ya kupangilia kazi zake, hivyo haitaathiri chochote kwa yeye kupewa timu ya taifa na huku akiwa kocha wa Azam FC, kwasababu hata sasa hajawahi kukosa mazoezini.

“Amekuwa na utaratibu mzuri, kama akifanya mazoezi na timu ya taifa asubuhi ujue jioni anakuwa na Azam FC, nikwambie ukweli hajawahi kukosa mazoezi ya Azam hata siku moja tangu amepewa Taifa Stars,” alisema Popat.

Alitolea mfano kwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, anayefundisha timu ya taifa ya DRC, huku bado anaendelea na majukumu yake ya klabu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*