googleAds

Ndayiragije apanga kuipiga mabao mengi Triangle United

NA GLORY MLAY

WAKATI Azam wakijiandaa kucheza na Triangle United  ya Zimbabwe katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam,  Kocha wa timu hiyo, Etienne Ngayiragije, amesema  wanahitaji ushindi mnono ili kujihakikishia kusonga mbele.

Akizungumza na BINGWA jana, Ndayiragije alisema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika.

Ndayiragije alisema wanahitaji walau ushindi  mkubwa wakiwa nyumbani kabla ya kwenda kucheza mechi ya marudiano.

“Wote mawazo yetu yapo kwenye mchezo ujao dhidi ya Triangle tunahitaji ushindi wa kwanza nyumbani kwa sababu tunajua ugenini ni ngumu kupata matokeo mazuri.

“Tunajua mchezo huo utakuwa mgumu lakini wachezaji wamejipanga katika nafasi zao kuhakikisha wanashinda, hivyo Watanzania waendelee kutusapoti,” alisema Ndayiragije.

Alisema wanaendelea na mazoezi katika uwanja wa Azam,  Chamazi na  wachezaji wake wapo fiti kwa mchezo huo.

Azam iliingia raundi ya kwanza ya michuano hiyo baada ya kuitoa Fasil Kenema ya Ethiopia kwa jumla ya ushindi wa mabao 3-2.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*