googleAds

Ndayiragije ahamishia silaha zake kwa Wazimbabwe

NA TIMA SIKILO

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Etienne Ndayiragije, amesema baada ya kukiongoza kikosi cha Taifa Stars kuitoa Burundi katika mechi za kusaka tiketi ya Kombe la Dunia, kwa sasa anahamishia mashambulizi kwa wapinzani wajao wa klabu yake hiyo, Triangle United FC ya Zimbabwe.

Azam FC watakutana na Triangle United FC katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaopigwa Septemba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana, Ndayiragije alisema hana muda wa kupoteza kwani mechi yao hiyo ya kimataifa inakaribia na wanahitaji kupata matokeo kwa njia yoyote, ukizingatia watacheza nyumbani.

“Tumebakiza siku chache, tarehe 15 sio mbali, nitajiunga na timu leo (jana) tuendelee kujiandaa na mchezo wetu wa mbele.

“Wapinzani ambao tunaenda kukutana nao tunawafahamu, tumeshawafuatilia na kuwaangalia wakicheza katika video zao mbalimbali,” alisema.

Aidha alisema anafahamu mchezo huo hautakuwa rahisi, lakini akiamini hakuna linaloweza kushindikana kwani malengo yao ni kupata matokeo mazuri.

Azam watakutana na Triangle baada ya kuwatoa Fasil Kenema ya Ethiopia katika hatua iliyopita ya michuano hiyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*