NATAMANI IDADI YA ‘MAPRO’ IONGEZEKE VPL

NA HASSAN DAUDI

KWA tathmini ya haraka na isiyohitaji uwekezaji mkubwa wa akili na nguvu, Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) ina wachezaji wengi wazawa kuliko wanaotoka nje ya nchi.

Kutokana na idadi yao ndogo, kulikuwa na uwezekano mkubwa wa wachezaji wa kigeni ‘mapro’ kufunikwa kabisa na wazawa.

Kinyume na matarajio hayo, hivi sasa mastaa wachache kutoka Burundi, Uganda, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, ndio wanaotawala soka letu. Kwani ni dhambi? Hapana.

Kutokana na kile wanachokifanya uwanjani, mashabiki wa kandanda wamejikuta wakivutiwa na wageni hao huku wakiwapuuzia kabisa wazawa.

Je, umewahi kujiuliza kwanini mashabiki wanavutiwa zaidi na mastaa Laudit Mavugo, Haruna Niyonzima, Thaban Kamusoko, Dornald Ngoma, Bukungu, Amis Kiiza, Amis Tambwe, Pascal Wawa ambaye ameondoka Azam? Nitakwambia.

Kilichonifanya nikaanzia huko ni mjadala mzito ambao umekuwa ukitikisa vichwa vya habari za michezo kwa miaka mingi, kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni Ligi Kuu Tanzania Bara inatakiwa kupungua.

Eti utitiri wa wageni umechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa soka la Bongo hasa mwenendo usioridhisha wa Taifa Stars.

Wapo wanaoamini kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni inatakiwa kupungua ili kutoa fursa kwa wazawa, wakisema wazawa wamekuwa wakikosa namba kwenye klabu zao, hivyo kushindwa kuitumikia vema Taifa Stars.

Hata hivyo, naamini kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kwa kuwa wazawa ameshindwa kufua dafu mbele yao haina tofauti na kitendo cha kumuua mtoto wa jirani eti kwa sababu ana maendeleo mazuri darasani kuliko mwanao!

Hapo unaweza kujiuliza, lipi suluhisho kati ya kumuua mtoto huyo wa jirani au kumsihi mwanao afanye juhudi kuhakikisha anajifunza kutoka kwake?

Binafsi siungi mkono wale wanaotamani kuona idadi ya wachezaji wa kigeni ikipungua na badala yake natamani waongezeke zaidi ya hawa waliopo hivi sasa.

Kusema wachezaji wa kigeni wanawazibia wazawa ni kuwalemaza wachezaji wetu ambao licha ya wingi wao ligi kuu wameshindwa kuwafunika wageni ambao wanahesabika.

Tunapaswa kukubali kuwa wanasoka wetu wameshindwa kuhimili ushindani wa namba kutokana na uvivu na kutoheshimu misingi ya kazi yao.

Ni wachezaji wangapi wazawa walishacheza kwa ustadi nafasi ya Niyonzima, Mavugo, Bukungu, Kamusoko, Twitte, Wawa, lakini wakavimba kichwa kutokana na sifa walizokuwa wakimwagiwa na mashabiki?

Wengi wao walionekana wazee kabla ya umri kusema hivyo. Hayo yalikuwa ni matokeo ya kuridhika, starehe, kupuuzia mazoezi na hata kutunishiana misuli na viongozi wao.

Hiyo ndiyo aina ya wachezaji wazawa tulionao na kwa mtindo huo ni ngumu kuota kuwa wataambulia chochote mbele ya wageni ambao silaha yao kubwa ni kujituma.

Kama idadi ya wachezaji wa kigeni itaongezeka zaidi, huenda ikaongeza ushindani na kuamsha wazawa ambao siku zote ni watu wa kuridhika kwa mafanikio kiduchu.

Ndiyo maana majina ya ‘mapro’ yamefanikiwa kuwa sehemu ya mazungumzo ya mashabiki wengi wa soka licha ya wingi wa wazawa ligi kuu.

Tofauti kubwa iliyopo ni kwamba, licha ya uchache wao, wachezaji wa kigeni wanajitoa zaidi na hiyo ndiyo silaha muhimu katika kujihakikishia namba kwenye vikosi vyao.

Wametamba na wanaendelea kutamba kutokana na udhaifu wa wachezaji wetu ambao kwa kiasi kikubwa hawajitambui.

Kwa upande mwingine, kuna hatari kubwa ya soka letu kudidimia zaidi kama idadi ya wachezaji wa kigeni itapungua. Labda wazawa watabweteka wakiamini kuwa wana nafasi kubwa ya kucheza kwenye timu zao. Hapo ndipo tutakapojikuta tukiiua kabisa Taifa Stars.

Tangu Tambwe alipotua nchini, amebaki kuwa kwenye ubora wake wa kupasia nyavu. Je, ni mshambuliaji gani wa Kitanzania aliyebaki kwenye kiwango cha juu kwa kipindi chote ambacho Tambwe amedumu Ligi Kuu Tanzania Bara?

Lakini pia, ikumbukwe kuwa idadi kubwa ya mapro wanaotua Ligi Kuu Tanzania Bara hutokea katika nchi zilizopiga hatua katika medani ya soka, hivyo bado tunawahitaji. Tofauti na wachezaji wa Tanzania, wengi huwa wamepikwa katika misingi imara ya soka la kisasa ikiwemo kupitia kwenye ‘academy’.

Ni rahisi kutabiri kuwa wamekuwa msaada mkubwa kwa wazawa ambao wamekuwa wakijifunza mambo mengi ya ndani na nje ya uwanja kutoka kwao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*