NA BADO

*Guardiola awajibu Mourinho, Sarri

*Adai dozi inaendelea, atawasukumia ndani mwanzo mwisho

MANCHESTER, England

KAMA ulidhani kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, atapunguza dozi ya vipigo kwa wapinzani, basi ulikuwa umekosea sana kuhusu hilo.

Guardiola bado anaonekana kuwa na kiu ya kuendelea kuweka rekodi mbalimbali ndani ya Ligi Kuu England ambayo inaaminika kuwa ngumu zaidi barani Ulaya.

Huu ni msimu wa tatu kwa kocha huyo raia wa Hispania na amefanikiwa kuifanya Manchester City kuwa timu hatari zaidi na yenye kuogopeka na wapinzani.

Hivi karibuni kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri, alisema kuwafikia Manchester City inatakiwa kuwe na uwekezaji mkubwa ndani ya klabu yake.

Pia, aligusia jinsi walivyo na wachezaji bora kila idara huku akikiri kuwa ngumu kwa timu nyingine kufikia muziki huo wa Guardiola ambaye anaonekana kuiweka Ligi Kuu England mikononi mwake.

“Kwa sasa Manchester City inahitaji uwekezaji mkubwa, kwani wana kocha na wachezaji wazuri, wana kila kitu bora,” alisema Sarri.

Naye Jose Mourinho baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Guardiola, alikiri kuwa itakuwa ngumu kuvunja utawala wa Manchester City bila kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wenye ubora.

“Unapoizungumzia Manchester City ni sawa na kusema juu ya mambo waliyoyafanya kwa miaka ya karibuni, hakuna kingine zaidi ya uwekezaji.

“Ni timu bora hivi sasa ili kuwafikia lazima timu nyingine zikubali kumwaga fedha kwa kusajili wachezaji nyota na wenye uwezo mkubwa,” alisema Mourinho.

Hata hivyo, Guardiola anaonekana kujibu mapigo hayo huku akisema bado ana kazi kubwa ya kuifanya ili apate timu anayoitaka, kwa maana hiyo hicho kinachoendelea England kinaendelea kupikwa.

“Wachezaji wangu wanafuata kile ninachotaka, nafurahi kwa hilo lakini bado tuna kazi kubwa huko mbele ya kuendelea kujenga timu yetu,” alisema Guardiola.

Hivi sasa Manchester City wanaongoza Ligi Kuu England baada ya kupigwa michezo 12, wakivuna pointi 32 wakifuatiwa na Liverpool yenye pointi 30 huku Chelsea ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 28.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*