MZIGONI

MUNICH, Ujerumani 

ULIMWENGU wa soka umemkumbuka aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, baada ya kukaa nje ya dimba kwa muda mrefu tangu alipoondoka Arsenal mwaka jana baada ya kushindwa kuipatia mataji timu hiyo.

Hata hivyo mambo huenda yakamwendea vizuri kocha huyo Mfaransa baada ya taarifa kuzagaa kwamba Bayern Munich imemtengea ofa nono ili achukue mikoba ya Niko Kovac aliyetimuliwa.

Kibarua cha Kovac kiliota nyasi mara tu timu hiyo ilipopokea kichapo cha kudhalilishwa cha mabao 5-1na Eintracht Frankfurt kwenye mechi ya Bundesliga wikendi iliyopita.

Wenger mwenye umri wa miaka 70 anatarajiwa kuzungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Bayern Munich, Karl- Heinz Rummenigge, wiki ijayo akitajwa kuwa chaguo sahihi wa kocha huyo wa zamani wa Frankfurt.

Imeripotiwa Bayern Munich ipo tayari kumpatia mkataba Wenger wa kukinoa kikosi hicho hadi msimu ujao, na itaangalia uwezekano wa kumchukua jumla.

Endapo Wenger atachukua nafasi ya Kovac, atashuka dimbani kwa mara ya kwanza kukiongoza kikosi hicho kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Tottenham utakaopigwa Desemba 11, mwaka huu.

Wenger ana uzoefu wa kufundisha timu zenye majina baada ya kuitumikia Arsenal kwa muda wa miaka 22, ikiwamo kuwanoa wachezaji vijana akiwemo Serge Gnbary, ambaye anakipiga Bayern.

Imefahamika Wenger alizikataa ofa kibao kukutoka timu mbalimbali tangu alipoondoka London, ikiwamo pia kuteuliwa kuwa  Mkurugezi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Alipoulizwa na kituo cha televisheni cha BeIN Sports endapo atakubali kazi hiyo ya ukocha, alisema, “Bila shaka nimemisi kazi yangu kwa muda mrefu, kuandaa timu kwa ajili ya mechi, kupata matokeo mazuri, hata hivyo nimefurahia maisha yangu nje ya kazi yangu pia.”

Mashabiki watasubiri kwa hamu mechi ya Bayern Munich dhidi ya Tottenham, ukiwa ni mtanange wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, endapo timu itakuwa chini ya Wenger, kutokana na kuifahamu vizuri timu hiyo kutoka London.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*