MZEE JENGUA: MIMI NI MWEMA, SANAA IMEFANYA NIONEKANE KATILI

KARIBU msomaji wa Jiachie na Staa Wako, safu inayokukutanisha na watu  maarufu kutoka sekta mbalimbali ndani na nje ya Bongo, ili upate kufahamu mambo mengi kutoka kwao, karibu.

Leo tupo na Mohammed Fungafunga maarufu kama Mzee Jengua, mkongwe wa sanaa ya uigizaji nchini akiwa amejizolea heshima kwa kuvaa uhusika wa mtu katili katika filamu zake ikiwamo tamthilia ya hivi karibuni inayoitwa Sarafu.

SWALI: Salim Musa wa Butimba, anauliza, unaweza kufanya filamu bure kutokana na ukongwe na heshima uliyonayo sasa?

Jengua: Nimekuwa nikitokea kwenye filamu nyingi sana kwa kuwa nimekuwa nikishirikiana na wasanii chipukizi japo mimi sisemi kama nchi hii tuna wasanii chipukizi, ila tofauti ni sisi wengine tumepata bahati ya kuonekana. Mimi naweza kucheza filamu bure ili kuwasaidia wasanii wachanga, ni lazima tukuze vipaji vipya kwa sababu sisi umri wetu umekwenda.

SWALI: Saudath Rashid wa Misufini, Morogoro, anauliza, huwezi kuwasahau wasanii gani kutokana na mchango wao waliokupa kwenye sanaa?

Jengua: Nikikumbuka zaidi ni wale ambao walinikuza nikiwa ndiyo naingia kwenye sanaa, ni wa kitambo kidogo kama vile Mzee Kipara, Mzee Rajabu Hatia, Pwagu na wengine ambao walitupatia ‘material’ zao bila tatizo na kufanya tuwe hivi leo.

SWALI:  Mkuta Mkuta wa Bugando Mwanza, anauliza, kwanini Kundi la Kidedea ambalo lilikuwa linarusha maigizo yake ITV lilikufa?

Jengua: Kidedea ulikuwa ni mchezo wa kuigiza ila kutokana na umaarufu wake, watu wakawa wanajua hata kundi linaitwa Kidedea, kundi lilikuwa linaitwa Chemchem Art Group, lilipotea kila msanii alipoanza kufanya mambo yake katika harakati za kutafuta maisha.

SWALI: Nashon Mlekwa wa Iringa anauliza, ni kweli wewe katili kama unavyoigiza katika filamu zako?

Jengua: Hapana, mimi ni mtu poa sana ila sanaa inanifanya nionekane vile kutokana na kuvaa uhalisia wa watu katili kwenye jamii. Mwongoza sinema akihitaji mtu mkali au katili lazima anifikirie mimi kwanza kwa sababu naweza kuigiza hivyo.

SWALI: Kylian Josea wa Mbande anauliza, kwanini kipindi hiki uonekane sana kwenye tamthilia kuliko kwenye filamu?

Jengua: Kazi ni kazi tu ilimradi mashabiki zangu wanapata kitu kizuri, asante Kylian kwa kunifuatilia na endelea kuburudika na tamthilia ya Sarafu na filamu nyingine ambazo nimeshiriki kuna mengi yanakuja, lakini pia tusisahau kuwa tamthilia zimerudi kwa kishindo baada ya kupotea kwa muda mrefu hivyo tuendelee kuziunga mkono.

SWALI: Neema Raishoba wa Bukoba anauliza, ukiwa kama mwigizaji mkongwe, je, ni lazima wasanii wa kike waigize kwa kuacha maungo yao wazi?

Jengua: Hapana, mimi ni miongoni mwa wasanii wanaolipinga hilo jambo, mbona sisi wazee tunacheza filamu bila kuacha wazi sehemu za miili yetu lakini bado tunaendelea kuwa na mashabiki wengi na filamu zetu zinanunuliwa, waache kwani wakiendelea hivi tusishangae pale ambapo filamu zetu zitadunda sokoni kwa sababu si kila mtu anafurahia vitendo vyao.

SWALI: Samweli 26 kutoka Kinondoni anauliza, kwanini wasanii wa zamani hamna mafanikio makubwa kama waliyonayo wa sasa?

Jengua: Kuna tabia kwa baadhi ya wasanii hawa vijana zinatukera sana sisi wazee au niseme sisi wakongwe, utakuta msanii kijana wanapeana mialiko yenye fedha tu lakini ile ambayo haina wanatuita kwa nguvu zote, si sawa kabisa hii ni tasnia yetu sote kwanini tusishirikiane kupeana dili ili tunufaike sote.

Wiki ijayo tutakuwa na Lulu Diva au Shilole, tuma swali lako kwao kupitia namba hapo juu, meseji tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*