MWIGULU AIFANYIA UMAFIA YANGA

HUSSEIN OMAR NA CLARA ALPHONCE


 

KUNA msemo unaosema mchawi ni nduguyo, hii ni baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa ni mmoja wa watu wanaoisaidia Yanga, kuifanyia umafia na kumsajili kiungo Awesu Ally wa Mwadui FC, kwa mkataba wa miaka miwili, kuitumikia Singida United msimu ujao.

Mwigulu, ambaye kwa sasa ni mmoja wa wamiliki wa Singida United, amewazidi kete Yanga kwa kuinasa saini ya mchezaji huyo, ambaye alikuwa kwenye rada za mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wa kihistoria nchini, wakiwa wamebeba ‘mwali’ mara nyingi zaidi ya timu yoyote nchini.

Yanga, wapo katika harakati za kuboresha kikosi chao na miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa na mpango nao, ni pamoja na Awesu, kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha kiungo huyo msimu huu.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga ambaye hakupenda jina lake kuwekwa hadharani, aliliambia BINGWA kuwa, wana majina ya wachezaji 10 wazawa ambayo watayajadili kabla ya kuanza kufanya mazungumzo, likiwamo la Awesu.

“Mambo yetu ni kimya kimya, tuna majina 10 ya wachezaji wazawa, hawa kwanza kabla ya kuanza nao mazungumzo, inabidi tujiridhishe ili kuepuka kuingia mkenge, tunataka kufanya usajili wa nguvu,” alisema.

Akizungumzia juu ya tetesi za kumtaka Awesu, mjumbe huyo alisema wamechelewa kufanya naye mazungumzo, kwani tayari yupo katika hatua za mwisho kusaini Singida United.

BINGWA lilimtafuta Awesu jana, ambaye alilithibitishia gazeti hili kuwa, msimu ujao atakuwa katika kikosi cha ‘walima alizeti’ hao wa Singida, kwani mazungumzo baina ya pande hizo mbili yanaendelea vizuri.

“Yanga na Singida wote walionesha nia ya kunihitaji, lakini nimeona Singida ndio wanakuja kwa kasi, siwezi kulaza damu, baada ya ligi kwisha nitasaini mkataba wa miaka miwili na timu hiyo, kila kitu kipo vizuri mpaka sasa,” alisema Awesu.

Huyu ni mchezaji wa pili kwa Singida kumsajili kimya kimya, baada kuinasa saini ya mchezaji wa JKU ya Zanzibar, Feithal Abdallah ‘Totoo’.

Alipoulizwa juu ya habari hizo za usajili, Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga, alikanusha kuwasainisha wachezaji hao, akidai kuwa, muda ukifika, wataweka wazi usajili wao.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Mwadui FC, Ramadhan Kilao, alisema kuwa, Awesu amebakiza miezi sita mkataba wake kumalizika, hivyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*