googleAds

Mwanza waanza kuandaa kikosi cha kikapu

NA BENJAMIN MASESE, MWANZA

UONGOZI wa Shule ya Sekondari ya Mwanza umeunda vikosi  tofauti vya timu ya mpira wa kikapu  itakayoshiriki michuano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza jijini hapa jana,  Makamu Mkuu wa shule hiyo,  Shukrani Lugaila,  alisema  uamuzi huo umetokana  na kujengewa uwanja wa kikapu wa kimataifa.

Lugaila alisema uwanja huo ulijengwa  na  Kampuni ya mafuta ya Moil kwa kushirikiana na wanafunzi  waliohitimu kidato cha nne mwaka 1968.

Alisema wakati wanafunzi hao wanahitimu mwaka 1968, shule  hiyo ilikuwa inaitwa Chopra,  ambapo mwaka huu  waliweza kukutana wakiwa katika mataifa mbalimbali na kurejea nchini kulipa fadhila zao.

“Leo hii wanafunzi wameupenda mchezo wa kikapu baada ya kujengewa uwanja huu, hata maradhi mbalimbali yaliyokuwa yakiwapata  yamepungua kutokana na kutojihusisha na michezo, kama uongozi wa shule tumemwandaa mwalimu wa michezo na tayari ameanza kuunda vikosi vya timu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

“Tunataka  ifikie wakati Serikali ikiwa na kikosi cha taifa cha timu ya kikapu inachukua wanafunzi wetu wengi tuliowaandaa kama ilivyo kikosi cha timu ya wanawake,  ambapo asilimia 90 ya wachezaji ni kutoka JKT Tanzania, ombi letu hapa ni kujengewa uwanja wa mchezo wa pete ili tuibue vipaji vya wanafunzi,”alisema.

Kwa upande wake, Mwalimu wa michezo, Abel Kalilo  alisema kabla ya kujengwa uwanja huo  hapakuwapo na hamasa ya mchezo wa kikapu.

 “Uwanja tumekabidhiwa na ulizinduliwa  Julai 22, mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella lakini ombi letu tunaomba Serikali imalizie kutujengea  vyumba vya kubadilishia nguo sambaba na vifaa vya michezo,” alisema Kalilo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*