MWANA FA, RICHIE MATUMAINI YA WASANII YAPO KWENU

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MWISHONI mwa wiki msanii wa muz58iki, Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’ na wa filamu, Single Mtambalike ‘Richie Richie’, walipata shavu katika bodi ya wajumbe wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Uteuzi huo ulifanywa na Waziri, Dk. Harrison Mwakyembe, ukiwajumuisha wajumbe wengine kama vile Mhadhiri wa Sheria Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Saudin J. Mwakaje, Mhadhiri Msaidizi Idara ya Sanaa Chuo Kikuu cha Dodoma, Asha S. Mshana pamoja na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk. Emmanuel M. Ishengoma, huku mwenyekiti wao akiwa ni Habbi Gunze.

Pongezi kutoka kwa wasanii wote wa filamu na muziki zimeelekezwa kwa Mwana Fa na Richie Richie kwa kuwa ndiyo watu maarufu zaidi katika bodi hiyo muhimu kwa uhai wa sanaa yetu.

Bila shaka Mwana Fa na Richie wanatambua kwanini wamepongezwa kwa kiasi kikubwa namna hiyo. Pongezi hizo zimebeba ujumbe, fukuto na matumaini waliyonayo wasanii.

Mfano wasanii wa Bongo Fleva kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika mawazo ya kisanaa waliyonayo kuminywa na baadhi ya sheria ndogo ndogo za baraza hilo.

Kama tunavyofahamu sanaa ina wigo mpana, msanii anapaswa kuwa na mawazo huru ya kuitekeleza sanaa yake bila kikwazo ili kufikisha ujumbe unaostahili kwa walengwa.

Sasa utaona hivi karibuni wasanii wamekuwa wakifungiwa nyimbo zao hata kama mtu kwa mawazo yake ‘binafsi’ ataona ina kasoro jambo ambalo linapunguza au kuua kabisa sanaa.

Hiyo yote ilitokana na hali ya hapo kabla kutokuwa na bodi yenye wajumbe wenye uhusiano wa moja kwa moja na sanaa kwa maana ya kuwa ni wasanii wanaofanya muziki na filamu.

Bila shaka Mwana Fa kwa muda wa miaka zaidi ya 10 aliyofanya Bongo Fleva, anafahamu changamoto zilizopo kwenye muziki hivyo uwepo wake katika bodi umekuwa faraja kwa wasanii wa muziki.

Hali kadhalika, Richie Richie ni mwingizaji mkongwe aliyeanza sanaa kipindi cha makundi ya uigizaji akitokea Nyota Ensemble akiwa na waigizaji wengine kama JB, Monalisa na Natasha zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Hivyo uwepo wa Richie Richie katika Bodi ya Baraza la Sanaa la Taifa umekuwa faraja kwa wasanii wa filamu ambao wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali zikiwamo za miundo mbinu ya sanaa yao.

Pia uwepo wa wasanii hawa maarufu katika bodi hiyo umeibua tumaini jipya kwa sanaa ambazo hazipewi nguvu japo kuwa wasanii wake wanaendelea kufanya kazi.

Sababu ikiwa ni uzoefu wa wajumbe hawa wawili, Richie Richie na Mwana Fa, katika biashara ya sanaa wakishirikiana na madaktari wenye uelewa mkubwa wa sanaa yetu kwa ujumla.

Uteuzi huo ulianza Oktoba 5 mwaka huu utawapa nafasi ya kuhudumia sekta ya sanaa nchini kwa muda wa miaka mitatu ijayo, huku matarajio yakiwa ni kutokea kwa mapinduzi makubwa katika upande wa mifumo wa uendeshwaji wa sanaa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*