googleAds

Mwakyembe aipongeza Kili Marathon kukuza utalii michezoni

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewapongeza waandaji wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa kukuza utalii katika michezo kupitia mbio hizo.

Dk. Mwakyembe alitoa pongezi hizo, wakati wa kikao maalumu na waandaaji hao kufuatia uzinduzi wa Kilimanjaro Marathon, uliofanyika mwezi uliopita, Dar es Salaam.

Waziri Mwakyembe aliamua kuwaalika waandaaji hao ofisini kwake, ili kujadili masuala mbalimbali ikiwamo namna ya kukuza riadha nchini, huku akiwataka wengine kuiga mfano huo.

Katika kikao hicho, kamati ya maandalizi ya Kilimanjaro Marathon iliwakilishwa na Mwaandaaji Mkuu, John Addison ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wild Frontiers.

Addison ndiye aliyebuni wazo la Kilimanjaro Marathon, Aggrey Marealle ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Executive Solutions kampuni inayoratibu mbio hizo kitaifa na mkurugenzi wa mbio hizo  John Bayo.

Dk. Mwakyembe alisema kuzingatia Kilimanjaro Marathon inashirikisha zaidi ya  watu 11,000 kutoka nchi 58 duniani kuna haja ya kuwapo ushirikiano wa karibu kati ya wizara yake na ile ya Maliasili na Utalii ili kukuza maendeleo ya michezo na utalii.

“Kilimanjaro Marathon imekuza utalii wa michezo kwa kiasi kikubwa, kwani washiriki wanaweza kutembelea vivutio mbalimbali vya kitalii katika Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine nchini na kuna vivutio vya utalii,” alisema.

Alisema riadha ni nzuri kwa afya, lakini pia ni moja ya chanzo cha fedha za kigeni kwa Tanzania.

Alitoa wito kwa mikoa yote inayoandaa mbio mbalimbali kuhakikisha wanazingatia faida ya mbio hizo kiuchumi kwa kuandaa shughuli za kitamaduni na kijamii kwa wenyeji na watalii kabla na baada ili kuongeza kipato na ajira.

Dk. Mwakyembe alionesha kufurahishwa na namna mbio mbalimbali zinaanzishwa mikoani, lakini akitoa tahadhari kuwa ni muhimu kuwapo na miongozo na vigezo  kuzingatiwa, huku akimtaka Mkurugenzi wa Michezo nchini kuhakikisha hili linasimamiwa kikamilifu.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe ametoa pongezi nyingine kwa waandaaji wa Kilimanjaro Marathon kwa kukubali kusaidia mbio za John Steven Akhwari zinatarajiwa kufanyika Juni, mwakani.

Waandaaji hao wanafanya kazi na wadau wengine wakiwamo Chama Cha Riadha Tanzania na Taasisi ya John Steven Akhwari ili kuweka vigezo mbalimbali  na kuhakikisha mbio hizo zinafanikiwa na kumtambua Akhwari ambaye anatambulika na Olimpiki.

Akizungumza kwa niaba ya waandaaji,  Marealle alimshukuru Dk. Mwakyembe kwa kuunga mkono mbio hizo  jambo ambalo limewapa heshima ya kipekee. 

@@@


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*