googleAds

MUZIKI WA ASILI NI DILI, TUUBEBE UTUBEBE KIMATAIFA

NA CHRISTOPHER MSEKENA

BONGO Fleva imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuteka kizazi kipya na kuwa faida kwa wasanii wake hususani kwenye suala zima la biashara, hawalii njaa kama wanavyolia wasanii wa sanaa nyingine tulizozisahau.

Lakini ukija katika utofauti wa muziki wa Bongo Fleva na miziki mingine ya duniani unagundua hakuna jipya, kukopi na kupesti kumekuwa kwingi hadi ladha ya Bongo Fleva inapotea, afadhali hivi sasa waandaaji wa muziki wanajitahidi kutengeneza midundo yenye vionjo vya asili vinavyosawiri Utanzania.

Utajiri mkubwa wa tasnia ya sanaa upo katika aina nyingine za muziki wa Kitanzania ambao hausikiki. Huenda sisi hatuoni lakini wenzetu wanaona na ndiyo maana msanii wa muziki wa asili akitoka kisanaa anatoka kweli kweli na maonyesho yake yanakuwa si na nchi hii, atafanya zaidi zake nyingi ughaibuni kuliko Bongo.

Miezi michache iliyopita nilipata wasaa wa kufanya mazungumzo na Msafiri Zawose, ambaye ni nyota wa muziki wa asili nchini na dunia inamtambua, tayari imempa heshima kubwa ambayo sisi huenda tumeshindwa kumpa kutokana na nguvu nyingi kuipeleka katika Bongo Fleva.

Katika mazungumzo hayo niliyofanya na Msafiri siku chache kabla hajakwenda nchini Marekani katika hafla ya utolewaji wa tuzo za Africa Magazine Music Awards (AFRIMMA) ambaye yeye alikuwa anawania kipengele cha Msanii Bora wa Muziki wa Asili barani Afrika, nilipata kujifunza mengi kuhusiana na utajiri wa muziki wa asili.

Inapendeza kuona mwaka huu nguvu kubwa ya Serikali imeelekezwa huko katika utamaduni wetu unaobebwa na muziki wa asilia katika matamasha ambayo yamekuwa yakileta chachu na mwamko wa jamii kuufuatilia muziki wa asili.

Mfano wa matamasha hayo ni lile la Urithi lililoratibiwa na Wizara ya Mali Asili na Utalii, hali kadhalika lile la Tulia Festival ambalo huratibiwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson yameleta mchango mkubwa katika kuendeleza muziki wa asili.

Mapokezi makubwa ya matamasha hayo katika mikoa tofauti ambayo yamepita, inatia moyo na inaonyesha namna gani muziki wa asili unapendwa. Vionjo vya Kiafrika ndani ya muziki vina upekee ambao hauwezi kupatikana popote pale, lakini pia utandawazi umetulazimisha kuuchukulia poa muziki huu.

Hapo ndipo tunaona wasanii kama Mrisho Mpoto wakifanya vizuri kutokana na kutumia udhaifu huo kuchanganya ladha za asili na Bongo Fleva hivyo kupata mapokezi makubwa kwa watu wa rika zote bila kujali utandawazi unaotutenganisha na asili zetu.

Tumezoea kuwaona wasanii wale wale kina Ali Kiba, Diamond Platnumz, Vanessa Mdee na wengine wengi wa Bongo Fleva, lakini kiu yangu kubwa ni kuona muziki wa asili nao unageuka na kuwa dili kwa kuingia kwenye mfumo wa kibiashara.

Ili wasanii wake wanufaike sawa na wale wa Bongo Fleva, lakini pia kusaidia kutengeneza utajiri wa urithi wetu kama Tanzania na Afrika huko duniani bila shaka tukiubeba muziki wa asili nao utatubeba pia katika anga za kimataifa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*