googleAds

Mtoto Pori kufuata nyanyo za Mzee Yusuf

Jeremia Ernest

MUZIKI wa mwambao umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuitangaza Tanzania kutokana na kubeba vionjo vya Kiafrika hasa maeneo ya Pwani ya Bahari Hindi.

Miongoni mwa waimbaji wa kiume wa muziki huo ni Mohamed Ally, maarufu kama Mtoto Pori aliyejizolea umaarufu kwa kushika nafasi ya Mzee Yusuf pale anapokosekana kwenye maonyesho mbalimbali kabla hajaacha muziki huo.

Katika mahojiano na BINGWA wiki iliyopita, mwimbaji huyo anasema kabila lake ni Mzaramo na alizaliwa mwaka 1983 katika hospitali ya Temeke na kupata elimu ya msingi Shule ya Keko Mwanga, jijini Dar es Salaam kabla ya kushindwa kuendelea na masomo.

Mtoto Pori alioa mwaka 2008 na amefanikiwa kupata watoto wawili.

ALIVYOINGA KWENYE SANAA

Anasema alianza sanaa katika kundi la ngoma za asili na muziki wa dansi lililokuwa likimilikiwa na msanii, Bakari Ndelema ‘Mzee Jangala’ ambaye ni mwalimu wake wa sanaa.

Anasema kwakuwa alikuwa anapenda na muziki wa taarabu, alilazimika kujiunga na kundi la Jahazi Modern Taarab ili aweze kuendeleza kipaji chake.

“Nilianza kuimba nyimbo za wasanii wengine katika bendi ya Steven Urembo aliyekuwa mpiga gitaa wa bendi ya Jahazi Modern Taarab,” anasema.

Mtoto Pori anasema Urembo ndiye aliyemfundisha jinsi ya kuimba muziki wa taarabu kama anavyoimba Alhaji Yusuf ‘Mzee Yusuf’ kwa sababu alikuwa ameshafanya naye kazi akiwa Jahazi.

Mwaka 2010 alishiriki katika shindano la nyimbo za taarabu lililoandaliwa na kituo cha radio, Times Fm na aliwashinda wasanii wengine 200.

“Niliposikia tangazo la shindano nilienda kuchukua fomu, tukaanza mchuano hatimaye nikaibuka kidedea hapo ndiyo Mzee Yusuf aliponiona,” anasema.

Anasema kipindi chote hicho alikuwa hajawahi kurekodi na kwa mara ya kwanza aliingia studio na bendi ya Jahazi kutengeneza wimbo ‘Yapwani Mitikisiko’, akaimba ubeti wa pili.

Baada ya muda, akaanza mazoezi na bendi ya Jahazi Modern Taarab, akapewa wimbo wa kwanza ‘Sumu Mpe Paka’ ambao ndio uliomtambulisha kwa mashabiki na kumpa umaarufu.

FAIDA, CHANGAMOTO ZA SANAA

Anasema faida kubwa aliyoipata katika sanaa ni kufahamiana na watu wa rika na kipato tofauti ambao kwa namna nyingine wamekuwa na faida katika maisha yake.

Aliweza kumudu maisha yake na familia kwa ujumla kwa kupitia sanaa na kwamba hakuwahi kufanya kazi wala biashara tofauti na muziki.

Kwa upande wa changamoto, anasema aliwahi kuzongwa jukwaani na mashabiki katika shoo yake ya kwanza jijini Dodoma alipokuwa akiimba wimbo wa Alhaji Mzee Yusuf.

“Shoo ya kwanza nilipanda jukwaani nikaimba wimbo wa Mzee Yusuf, mashabiki wakaleta fujo wakisema naimba kwa CD, kwakuwa sauti haikuwa na tofauti,  ikabidi aje mwenyewe ili kuwatuliza mashabiki na kuwafafanulia kuwa ni kijana ninayefuata nyayo zake,” anasema Mtoto Pori

Changamoto nyingine ni kukosa nauli wakati akiwa katika kikundi cha ngoma za asili kwa sababu walikuwa hawalipwi.

KILICHOFANYA AKAE KIMYA

Ameeleza safu hii kuwa bendi ya Jahazi Modern Taarab ilikuwa na wasanii wengi hivyo kupewa wimbo inachukua muda mrefu ndiyo maana akawa hasikiki.

Anasema sababu nyingine ni kustaafu kwa Alhaji Mzee Yusuf kuimba muziki huo.

“Toka Mzee Yusuf aache muziki, bendi iliyumba pia muziki kwa ujumla umeshuka siyo kama zamani ndiyo maana wasanii wengi wa Taarab tuliokuwa Jahazi hatusikiki kama zamani,” anasema.

YUKO WAPI NA MIPANGO YAKE

Anasema anaishi Vingunguti na familia yake na bado anafanya muziki katika bendi mpya ya First Classic iliyo chini ya Prince Amigo.

Pia, yupo katika mchakato wa kutoa nyimbo zenye mahadhi ya mduara kwasasa bado zipo jikoni muda si mrefu atazitambulisha kwa mashabiki.

Anasema kitu anachojivunia katika maisha ni mke ambaye wamepita vikwazo vingi ila amekuwa mvumilivu huku moja ya mipango yake ikiwa ni kufanya sherehe ya kumbukizi ya miaka 10 ya ndoa yao jambo ambalo siyo rahisi kwa mtu maarufu.

Anaongeza kuwa ikitokea amepata fedha za kuanzisha biashara ambayo inaweza kumwingizia kipato cha kuendesha familia, ataacha kuimba muziki wa Taarab na kufuata nyayo za Alhaji Yusuf.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*