googleAds

MTAZAMO POLISI DODOMA MNAWEZA KAZA BUTI

NA MOHANMED HAMMIE

LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara  imefika ukingoni huku tayari mwelekeo wa timu zitakazopanda daraja kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara zikiwa zimeanza kujulikana.

Timu ambazo ziko katika mazingira bora ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, ni Lipuli ya Iringa inayongoza Kundi A, kutokana na pointi 26,  Singida United inayoongoza Kundi C, kwa pointi  26 na  Njombe Mji ya Iringa, Polisi Moro na KMC ya Kinondoni ambazo zinaongoza kwa Kundi B, kutokana na kila moja kufikisha pointi 19.

Kwa upande wa Polisi Dodoma, hawa kwa mara nyingine tena wameshindwa kuikaribia ligi kuu kutokana na kuendelea kufanya vibaya katika mechi zao.

Licha ya kushindwa kupangilia mikakati yao ya kurejea kwenye ligi hiyo, lakini msimu ujao wameweza kuonyesha uwezo wa kusakata kabumbu na kufanikiwa malengo ambayo watakuwa wamejiwekea.

Polisi Dodoma wamecheza mechi 11 na wamefikisha pointi 13 ikiwa ni tofauti ya pointi 15 dhidi ya Singida United  wanaoongoza kwenye kundi lao C.

Pongezi kwa hapo walipofikia, kwani msimu huu wa Ligi Daraja la Kwanza  ulionekana kuwa na ushindani mkali  tofauti na misimu mingine iliyopita.

Lakini ukiachilia mbali na upungufu ulioonyeshwa na waamuzi kwa kushindwa kutafsiri vema sheria 17 za soka, lakini timu zilionyesha kandanda safi kutokana na ubora wa vikosi vyao.

Ni wazi kwenye michezo saba ya mwanzo kila mdau wa soka alionekana kuvutiwa na ligi hiyo huku akishindwa kutabiri nani angeweza kupanda daraja msimu huu.

 

Ushindani wa soka ulionekana hata kwa Polisi Dodoma walianza vizuri kwa kushinda mechi zao na kuingia katika nafasi tano bora kati ya mechi 11 walizokuwa wamecheza na kushika nafasi ya nne kwenye kundi lao.

Nina hakika Polisi Dodoma wanaweza kurejea Ligi Kuu Bara kutokana na kandanda safi walilolionyesha msimu huu na kuweza kurejesha hadhi ya mkoa huo kisoka kama ilivyokuwa CDA miaka 10 iliyopita.

Kizuri zaidi kwa Polisi Dodoma ndio Mji Mkuu  wa Tanzania na Rais John Pombe Magufuli, ameshaweka mikakati ya kujenga uwanja mkubwa wa soka kupitia kwa ufadhili wa Mfalme wa Maroco,  hiyo ni nafasi nzuri kwa timu za Dodoma kuonyesha wanaweza kucheza katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ingawa msimu huu wamekosa nafasi hiyo, bado wana nafasi ya kuingia Ligi Kuu Tanzania Bara iwapo kama wataweza kujipanga upya kwa kufanya usajili makini na kupata benchi bora la ufundi.

Kila kitu ni nia na mipango, hivyo basi Polisi Dodoma wasikate tamaa ni wakati wa kuangalia wapi walipokosea na kujipanga upya, hakika Polisi Dodoma wanaweza ni muda wa kukaza buti kuanzia sasa kuelekea msimu ujao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*