googleAds

Msuva atimua kocha Morroco

NA ZAINAB IDDY

UONGOZI wa klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco umemfuta kazi kocha wake, Sebastian Desabre baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya DifaĆ¢ El Jadida ya nchini humo.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Morocco (Botola) walipoteza mchezo huo uliochezwa wikiendi iliyopita kwa bao lililofungwa na winga wa timu ya Taifa ya Tanzania, Simon Msuva.

Msuva aliibuka shujaa dhidi ya vigogo hao ambao ndio walikuwa wenyeji wa mtanange huo kwa kupachika bao hilo la ushindi kwenye dakika ya 20 kupitia shambulizi la kushtukiza.

Mara baada ya mchezo huo, Wydad Casablanca ilitoa taarifa jana kupitia mtandao wake na kuthibitisha kuwa imemtimua kazi kocha Desabre, ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu impe tena kibarua, Januari 15 mwaka huu.

Desabre ambaye ni kocha wa zamani wa Pyramids ya Misri na timu ya Taifa ya Uganda, anaondoka Wydad akiacha mkataba wa miaka miwili ambao aliusaini wakati anarejea hapo.

Kocha huyo anaondoka akiwa na rekodi ya kushinda michezo mitatu, sare moja na kichapo kimoja dhidi ya Difaa El Jadida.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*