googleAds

MSIHOFU, TUPO VIZURI UGENINI

TIMA SIKILO

WAPENZI wa Yanga, wametakiwa kutokuwa na hofu na kikosi chao, kwani wana wachezaji wenye uwezo wa kufanya makubwa msimu ujao, wanaohitaji nguvu kidogo tu iliyopo ndani ya uwezo wa Kocha Mkuu wao, Mwinyi Zahera.

Baada ya kukishuhudia kikosi chao kikitoka sare ya bao 1-1 na Kariobangi Sharks ya Kenya na Township Rollers ya Botswana, wapenzi wa Yanga wameonekana kuanza kuvunjika moyo, wakiamini msimu ujao huenda ukawa wa maumivu tena kwao.

Mchezo dhidi ya Kariobangi Sharks, ulikuwa ni wa kirafiki uliochezwa Agosti 4, mwaka huu, siku ya kilele cha Wiki ya Wananchi, wakati ule na Rollers ni wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, zote zikipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa kiasi kikubwa, wapenzi wengi wa Yanga walionekana kutoridhishwa na muunganiko wa kikosi chao, wakimtupia lawama Zahera kutokana na kitendo chake cha kuchelewa kurejea nchini kuwapika vilivyo vijana wake.

Kwa kufahamu hilo, Zahera amevunja ukimya akiahidi kulifanyia kazi tatizo ndani ya siku zilizobaki kabla ya kurudiana na Rollers, ugenini kati ya Agosti 24 na 25, mwaka huu.

Kocha huyo ameliambia BINGWA kuwa kikosi chake kinatarajiwa kuondoka leo jijini Dar es Salaam kuelekea Moshi ambapo wataweka kambi ya siku chache kufanyia kazi kasoro zote zilizojionyesha kwa timu yake, lakini zaidi ikiwa ni kutengeneza muunganiko wa vijana wake, kuanzia safu ya ulinzi, kiungo hadi ushambuliaji.

Alisema wakiwa Moshi, watacheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Tanzania Prisons na AFC Leopards ya Kenya, kwenye Uwanja wa Ushirika.

“Kikosi chetu chote kitasafiri kuelekea Moshi, kabla ya kuelekea Botswana. Kikosi kipo salama kasoro Paul Godfrey peke yake ambaye aliumia katika mchezo uliopita,” alisema.

Aidha, Zahera alisema bado baadhi ya wachezaji wao vibali havijakaa sawa hivyo katika lango lake, anaweza kuendelea kumtumia Metacha Mnata kwani yuko vizuri, akikiri hata mchezo uliopita, hakufanya makosa.

“Hata wachezaji wengine, walicheza vizuri, tatizo limebaki kwetu benchi la ufundi, kuwaunganisha, hilo tutalifanya kazi ndani ya siku chache zilizobaki,” alisema.

Juu ya hofu waliyonayo wapenzi wa Yanga kuelekea mchezo wao wa marudiano dhidi ya Rollers, Zahera alisema: “Mashabiki wasisahau kwamba msimu uliopita tuliweka rekodi nzuri katika viwanja vya ugenini, basi tuna nafasi kubwa ya kushinda hata tukiwa Botswana.”

Alisema Township Rollers walifanikiwa kuwabana Jumamosi iliyopita kwa kuwa wageni wao hao waliwasoma mapema katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Kariobangi Sharks, hivyo kuahidi kwenda kuwashikisha adabu kwao.

Juu ya winga wake, Patrick Sibomana aliyekosa penalti ya kwanza kabla ya kurekebisha makosa yake wapopata adhabu hiyo kwa mara ya pili, alisema: “Katika upigaji wa penalty, nilikuwa nimeshapanga atapiga Patrick Sibomana na mwingine ni Juma Balinya, nilipoona (Sibomana) amekosa ile ya kwanza, nikamwambia arudie ili kumrudisha katika hali yake ya kawaida na niliamini atafanya vizuri.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*