googleAds

MSEKWA MGENI RASMI MWALIMU NYERERE MARATHON

NA MWANDISHI WETU

SPIKA Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha la kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere litakalofanyika Oktoba 14, mwaka huu, Butiama mkoani Mara.

Tamasha hilo lililopewa jina la Mwalimu Nyerere Historical Marathon, litahusisha mchezo wa riadha ambapo wanariadha wa wilaya za Bunda, Serengeti, Musoma, Butiama na mikoa ya jirani watachuana.

Mbali na riadha, tamasha hilo pia litahusisha michezo ya mbio za baiskeli, bonanza la mpira wa miguu na mkesha wa kusifu na kuabudu.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mratibu wa tamasha hilo, Kulwa Karedia, alisema lengo la kuandaa tamasha hilo ni kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika kupinga udhalimu wa wakoloni na hatimaye kuiletea Tanzania uhuru.

“Tumeamua kuandaa tamasha hili kwa lengo la kuenzi kwa vitendo mchango wa Mwalimu Nyerere ambaye ni mwasisi wa Taifa letu kutokana na kujitoa kwake kupingana na Serikali ya kikoloni hadi kufanikisha kupatikana kwa  uhuru ambao kila mmoja wetu anaufurahia leo hii.

“Sisi kama vijana tumeona kuja haja ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kumuenzi mwasisi wetu, wakati maadhimisho ya kitaifa yakifanyika Tanga, tumeona ni vema na sisi tumuenzi kivingine ili kuleta umoja wa kitaifa,” alisema Karedia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Kuhifadhi Utamaduni wa Wazanaki, Mashaka Mgeta, alisema tamasha hilo linalenga kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere wa kuiunganisha Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Jambo hilo si la mzaha, kwani linachagiza kuleta muungano wa kitaifa, tamasha hili lina malengo mapana ya kuiunganisha Afrika kiumjula, kwani mwalimu atakumbukwa pia kwa mchango aliutoa kwa nchi nyingi za Afrika, hasa Kusini mwa Afrika kupata uhuru,” alisema Mgeta.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*