Msala:Messi adai Copa Amerika rushwa tupu, akipigwa ‘red’

RIO, Brazil

MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, amekijia juu Chama cha Soka America Kusini (Conmebol) kupitia marefa wake, akidai kuna vitendo vya rushwa vya chini chini vilivyojionyesha katika michuano ya Copa America ya kila mwaka.

Kauli hiyo imewashtua mashabiki wengi wa soka duniani na kuzua gumzo, baadhi yao wakidai pengine huenda nyota huyo amepatwa na hasira baada Argentina kung’olewa katika michuano hiyo na kushindwa kusonga mbele.

Mwanandinga huyo alitoa povu baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu ambayo imedaiwa si ya kihalali kutokana na kutunishiana misuli na mchezaji wa Chile, Gary Medel katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.

Hata hivyo, Argentina ilitoka kifua mbele kwa kuichapa Chile mabao 2-1 kabla ya kuingia kwa dosari ya tukio hilo katika mtanange huo.

Argentina imejikuta ikiishia nafasi ya tatu ya baada ya kutolewa na wenyeji, Brazil, kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0 wiki iliopita.

Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita, Messi aliwahi kusema kuwa Brazil inapendelewa na marefa kwakuwa wao ni wenyeji wa michuano hiyo, wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele.

Hata hivyo, Conmebol imepingana na kauli hiyo na kutoa tamko kuhusiana na kashfa hizo zilizotolewa na Messi ambaye anakipiga katika klabu ya Barcelona, wakisema ni kinyume na misingi ya sheria ya michuano.

Akizungumza baada ya mtanange wao dhidi ya Chile, Messi alisema hawatakubali kuwa sehemu ya vitendo hivyo vya rushwa.

“Hatuwezi kuwa sehemu ya rushwa katika michuano hii, hawakuonyesha heshima kwetu, marefa wameharibu soka kwa mchezo mchafu, wamezingua sana,” alisema Messi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*