googleAds

MSAFIRI ZAWOSE ATOA SIRI YA WAZUNGU KUUPENDA MUZIKI WA ASILI

INATOKEA mara chache sana hapa Bongo kwa msanii wa muziki wa asili kupata nafasi ya kushiriki kwenye tuzo kubwa za kimataifa, tumezoea kuona wakali wa Bongo Fleva kama vile Ali Kiba, Diamond Platnumz, Vanessa Mdee na wengineo wakituwakilisha vyema huko ugenini.

Kwa maana hiyo tunapoona msanii wa muziki wa asili amepata nafasi ya kuliwakilisha Taifa kwenye kinyang’anyiro chochote kile hatuna budi kumuunga mkono ili tumpe nguvu ya ushindi kwa umoja wetu kama mashabiki wa muziki.

Jiachie na Staa Wako leo nakukutanisha na staa wa muziki wa asili nchini, Msafiri Zawose ambaye muziki wake umefanya aizunguke dunia na kushiriki kwenye matamasha makubwa na warsha mbalimbali kwenye nchi kama Marekani, Uingereza, Ujerumani, Uarabuni, Uganda, Kenya na kwingineko.

Msafiri ambaye ni mtoto wa mwasisi wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo, Dk. Hukwe Zawose, ni Mtanzania pekee anayewania tuzo za All Africa Music Awards (Afrima 2017) zitakazotolewa Novemba 12, mwaka huu nchini Nigeria katika kipengele cha Mwimbaji/Kundi Bora la muziki wa asili kupitia ngoma yake inayoitwa asili yetu, karibu ufahamu mengi kutoka kwake.

SWALI: Tunaona vijana wengi kama wewe wanajikita zaidi kwenye Bongo Fleva, sababu gani imefanya uchague muziki wa asili?

Msafiri: Nafanya muziki wa asili kwa sababu naupenda na ni utambulisho wangu na ninaweza kufanya mtindo wowote kupitia muziki huu wa asili.

SWALI: Unadhani kwanini vijana wa kisasa wanapenda kufanya Bongo Fleva zaidi na si muziki unaofanya wewe?

Msafiri: Binafsi naona vijana wengi wanajiingiza kwenye muziki wa Bongo Fleva kutokana na mfumo na ‘platform’ iliyopo na pia hawatambui umuhimu na thamani kubwa ya muziki wa asili, kutokana na uwezo walionao ni ngumu kutambua umuhimu na namna ya kuendeleza muziki wa asili kupitia vipaji vyao.

SWALI: Una mpango gani kuhakikisha muziki wa asili unakuwa ni biashara kama zilivyo aina nyingine za muziki?

Msafiri: Mpango ninaoufanya ili uwe wa kibiashara ni kutengeneza miundombinu na namna gani ya kupiga ukawa unatambulika kwenye masoko makubwa ya kidunia, kuufanya ukue ni kuupiga katika namna mbalimbali, katika mitindo na mirindimo mbalimbali ya kidunia.

SWALI: Mafanikio gani umeyapata kupitia muziki wa asili?

Msafiri: Mafanikio makubwa niliyoyapata ni kuweza kupenya na kuingia kwenye soko kubwa la kiulimwengu kupitia muziki wa asili, kupata kipato na kutanua wigo mpana sana kupitia sanaa zetu na pia nimetengeneza mtandao mkubwa sana wa kidunia.

SWALI: Mashabiki wengi wa bidhaa yako ya muziki wa asili ni raia wa kigeni (wazungu), unadhani kwanini ni hao na si Watanzania/Waafrika?

Msafiri: Wazungu wanapenda kwa sababu wanaona ni kitu tofauti  na hakifanani na kitu chochote na wanaamini muziki wangu ni tofauti katika ulimwengu na una mahadhi ambayo yananitambulisha mahali ninapotoka na kwa sisi Waafrika hatujithamini na kujitambua kutokana na mfumo unaosababisha kuwe na msukumo mdogo sana wa kusukuma muziki wa asili kutokana na uelewa na utumwa wa mawazo.

SWALI:  Mashabiki zako watarajie nini kipya kutoka kwako?

Msafiri: Mipango yangu ni kuhakikisha muziki wa asili unatambulika kidunia na hapa nyumbani, projekti mpya nimeingiza muziki wa asili katika viwango vikubwa vya kimataifa na kutengeneza mfumo wa kusikilizwa na kila aina ya mtu duniani.

SWALI: Hivi sasa upo kwenye tuzo za Afrima kama Msanii Bora wa Muziki wa Asili Afrika, Watanzania wanaweza kukupigia kura kwa njia ipi?

Msafiri: Kwa sasa unaweza kunipigia kura kupitia tovuti yao ya www.afrima.com  ukiingia hapo kupitia intaneti utakwenda moja kwa moja kwenye kipengele cha Best Artist In Traditional Music, utabonyeza jina langu utakuwa umenipigia kura.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*