googleAds

MRITHI WA MAKAMBO ATUA

NA MWAMVITA MTANDA

STRAIKA mpya wa Yanga anayepewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya Heritier Makambo katika kucheka na nyavu, Tariq Seif, ametua nchini jana alasiri tayari kumalizana na Wanajangwani hao.

Seif aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 9:30 alasiri, akitokea Misri alikokuwa akikipiga katika klabu ya Dekernes FC ya Misri.

Akiwa na kikosi hicho cha Dekernes FC, Seif alifanikiwa kufunga mabao saba ndani ya mechi saba na kutoa pasi tatu za mabao (assist) kuonyesha jinsi alivyo mkali wa kucheka na nyavu.

Lakini pia, ikumbukwe kuwa Seif alishaanza kuonyesha makali yake katika ufungaji tangu alipokuwa hapa nchini, zkifanya hivyo katika timu mbili alizozichezea Ligi Kuu Tanzania Bara, Stand United na Biashara United.

Akiwa na Stand United ya Shinyanga, alifunga mabao manne Ligi Kuu Bara kabla ya kucheka na nyavu mara sita alipoitumikia Biashara United ya Musoma.

Makali yake hayo ndiyo yaliyomfanya kuwavutia Dekernes FC na kuamua kumsajili.

Akizungumza baada ya kutua uwanja wa ndege jana, Seif alisema pamoja na kuendelea kutakiwa na Dekernes FC, amependa kurejea Tanzania baada ya Yanga kuonyesha nia ya dhati ya kuhitaji huduma yake.

Alisema binafsi ameona ni vema kurejea nchini kuitumikia Yanga kwa kipindi hiki ambacho mashabiki wake wanaonekana kuwa na kiu ya mabao, akiamini atawafurahisha.

“Tanzania ni nyumbani kwetu, nimejifunza mengi Misri, naamini huu ni muda mwafaka kurejea nyumbani kuitumikia timu ya kwetu. Yanga wamenihitaji, hivyo naamini hata nikiwa hapa, ninaweza kufika mbali kama ilivyokuwa kwa Simon Msuva na wengineo,” alisema Seif, mwenyeji wa Tanga.

Kwa upande wake, mmoja wa vigogo wa Yanga, alisema kuwa tayari wameshafanya mazungumzo na mchezaji huyo na juzi walimtumia tiketi ya ndege ili waje wamalizane naye.

Alisema japo uongozi wa Dekernes bado ulikuwa ukimuhitaji mshambuliaji huyo, lakini meneja wa mchezaji huyo ameona ni vema mteja wake kutua Jangwani akiamini nako ni sehemu ya sahihi ya kumfikisha mbali kutimiza ndoto yake ya kucheza Ulaya.

“Yule mchezaji ni hatari ndio maana Waarabu walimchukua. Tupo tayari kumsajili kwa gharama yoyote na kesho (leo) anasaini mkataba.

“Tumeona mapungufu kwenye safu yetu ya ushambuliaji toka alipoondoka Makambo, sasa huyu ni mtoto wa nyumbani, lazima atafanya makubwa, kwanza ni mdogo halafu ana hasira na hizi timu kubwa,” alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda jina lake kuwekwa wazi.

Juzi Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alikiri klabu yao kutumia tiketi za ndege wachezaji kadhaa, akiwamo Seif ili kukiimarisha kikosi chao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*