Mpira Pesa Original yajipanga kutengeneza bonge la ofisi

WINFRIDA MTOI

MPIRA Pesa ni miongoni mwa matawi ya mashabiki wa Klabu ya Simba yenye nguvu kubwa hapa nchini kutokana na ukongwe wao ikiwemo kushiriki mambo mbalimbali yanayohusu timu.

Tawi hilo limekuwa na nguvu na ushawishi mkubwa kwa Wanasimba kutokana na wanachama wake kuwa na msimamo wa kufanya mambo yao bila kuendeshwa na mtu.

Tumeshuhudia mara kwa mara, Mpira Pesa wakipewa nafasi kubwa katika shughuli nyingi za klabu hiyo, hali inayosababishwa na misimamo ya viongozi wake na wanachama.

Hata katika chaguzi mbalimbali za Simba, Mpira Pesa imekuwa ni tawi linalopenda kusimamia misimamo yake ambayo wanaona itakuwa na faida kwa klabu pamoja na mashabiki.

Kwa kudhihirisha ukongwe wa tawi hilo na misimamo yake, liliwahi kutoa mwenyekiti ambaye ni Hassan Dalali kuiongoza Simba miaka ya nyuma.

Hata hivyo, hivi karibuni tawi hilo liliingia katika mgogoro na kusababisha wanachama wake kugawanyika na kuzaliwa matawi mawili, moja likijiita Mpira Pesa Group ambalo lipo chini ya Dalali na wengine kubaki tawi la zamani wakijiita Mpira Pesa Original.

Mgawanyiko huo ulitokea kipindi cha mchakato wa mabadiliko kutokana na kupingana kati ya wale wanaohitaji mabadiliko na wasiotaka mabadiliko.

BINGWA katika safu yake ya Tawi kwa Tawi, limefanya mahojiano na Katibu Mkuu wa tawi la Mpira Pesa Original, Suleiman Kitambi, aliyeelezea maendeleo ya tawi hilo baada ya mgawanyiko na hali ya wanachama ilivyo.

Kitambi anasema changamoto waliyoipata kipindi hicho cha kugawanyika ilikuwa ni kubwa, lakini kwa sasa wamesimama vizuri na wameanza mchakato wa kutengeneza ofisi mpya baada ya ile ya awali kubomolewa.

Anasema ofisi zao za siku zote zilikuwa zipo Magomeni Mikumi, lakini kutokana na mgawanyiko uliotokea, eneo hilo likachukuliwa na wenyewe na kutakiwa kubomoa ofisi hiyo.

Kitambi anasema kwa sasa hali imetulia na wameshafanya uhakiki wa wanachama waliobaki nao ambao wanafika 176, hivyo kilichopo katika mipango yao ni kutengeneza ofisi.

Anasema tayari eneo la kuweka ofisi wamelipata ambayo itakuwa maeneo ya hapo hapo Magomeni Mikumi na wamejipanga kuhakikisha ndani ya miezi miwili imekamilika na kuizindua.

“Tumepitia changamoto katika kipindi hiki cha mgawanyiko uliosababishwa na wanachama ila tayari tumefanya uhakiki na kubaini tuliobaki ni kama 176 ikiwemo kikundi cha ngoma na hii  inatosha kusapoti timu yetu.

“Suala kubwa tunaloliangalia kwa sasa ni kutengeneza ofisi ili kuwaunganisha wanachama wetu kila mmoja apate kadi halali ya uanachama wa klabu ya Simba.

“Tunashukuru mwenendo wa tawi unakwenda vizuri, kwa sasa hakuna tena matatizo na hata wale wenzetu waliokuwa wanapinga mabadiliko hadi kuondoka, wamekubaliana na hali ya uendeshaji wa klabu yetu,” anasema Kitambi.

Anasema Mpira Pesa Original ni tawi linalojivunia mabadiliko ya Klabu ya Simba kwa sababu walipambana kipindi chote cha mchakato hadi kupitishwa kwa mfumo huo wa uendeshaji wa klabu.

“Moja ya vitu tunavyojivunia ni kupigania mabadiliko na yamepatikana, mafanikio ya timu yetu yametokana na mabadiliko hadi tumeweza kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu,” anasema Kitambi.

Anaeleza kuwa harakati zao bado zinaendelea katika kuisapoti timu yao kila mahali na kuhakikisha baada ya mechi mbili wameshatangazwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tuna matumaini makubwa ya kutetea ubingwa wetu, tuna mechi nyingi mkononi kuliko wenzetu, hivyo nguvu zote tumeelekeza kwa timu yetu ili kuchukua pointi katika michezo iliyobaki,” anasema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*