Mpango mzima Simba huu hapa

NA WINFRIDA MTOI

JAPO Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu bado haijamalizika, kwa sasa mabosi wa Simba wameshahama katika kipute hicho na badala yake, akili zao zote zikiwa ni kwenye mioyo ya wapenzi wao kuona ni vipi wanawapa raha zaidi.

Mabosi wa Simba wanafahamu kuwa kiu ya wapenzi wa klabu yao si kuifunga Yanga kwani wameshawahi kuwachakaza vibaya mno watani wao hao wa jadi, kikiwamo kipigo cha kihistoria cha mabao 6-0 mwaka 1977.

Wanachofikiria viongozi wa Simba kwa sasa ni jinsi ya kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika au hata lile la Kombe la Shirikisho barani humo kwani hiyo ndiyo kiu kubwa ya mashabiki na wanachama wao.

Kwa kutambua hilo, viongozi wa Wekundu wa Msimbazi hao kwa sasa wanaumiza vichwa jinsi ya kufanikisha hilo, wakianzia na jinsi ya kukisuka zaidi kikosi chao, kabla ya kuelekea maeneo mengine ya ndani na nje ya uwanja.

Katika hilo, tayari Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameomba kupewa faili la wachezaji ambao hawahitajiki kikosini mwao ili waweze kumalizana nao mapema.

Lakini pia, benchi la ufundi lilitakiwa kuwasilisha ripoti kamili inayohusisha pia usajili wa msimu ujao, ili uweze kufanyiwa kazi, huku wachezaji wanaolengwa wakiwa ni wale wa kuwawezesha kuitikisa Afrika.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa tayari mpango mzima wa klabu hiyo kuelekea ushiriki wao wa michuano ya kimataifa msimu ujao upo mezani kwa Mo Dewji ambaye anaupitia kwanza kabla ya kuupeleka mbele ya Bodi ya wakurugenzi ili kuufanyia kazi.

Na kwa kuwa kwa sasa shughuli za mikusanyiko zimesimamishwa na Serikali kama sehemu ya kudhibiti kusambaa kwa virus vya ugonjwa hatari wa Corona, Mo Dewji na wenzake wanatumia fursa hiyo kuona wanatokaje, ili kipute cha Ligi Kuu kikirejea, wawe wamemaliza kazi na kubakiwa na maandalizi ya sherehe za ubingwa wa Bara.  

Japo tayari Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, ameshaanika baadhi ya wachezaji ambao hawapo katika mpango wake wa msimu ujao, akiwataja Wabrazil, Gerson Fraga na Tairone Santos Da Silva, lakini bado mabosi wa klabu hiyo wanaamini wapo nyota wao ambao muda wao wa kuendelea kukipiga Msimbazi umekwisha.

Hivyo, mkakati wao ni kukibomoa kikosi chao na kusuka kipya kitakachoweka historia Afrika, ukizingatia tayari walishawashtua wadau wa soka barani humo pale walipotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha, ameshaweka wazi kuwa kwa sasa wanaifanyia kazi ripoti ya kocha wao, Sven Vandenbroeck.

“Tumeshaipokea ripoti ya mwalimu na sasa tunaifanyia kazi, hili si suala la kutangaza hadharani, likikamilika tutawajulisha kila kitu,” alisema.

Alisema azma yao ni kusajili wachezaji wenye hadhi ya michuano ya kimataifa, wakitupia macho yao ndani ya nchi na kwingineko kutegemea na mahitaji ya kikosi chao.

“Lengo letu ni kubakiwa na wachezaji wenye uwezo wa kutufikisha pale tunapotarajia, hasa mafanikio katika michuano ya kimataifa na si vinginevyo. Tulifika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, kwa sasa malengo yetu ni kuvuka hatua hiyo, hilo lipo ndani ya uwezo wetu,” alisema Senzo.

Hadi Ligi Kuu Bara inasimamishwa kutokana na hofu ya virus vya Corona, Simba iliyoshuka dimbani mara 28, inashikilia usukani wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 71, ikiziacha kwa mbali Azam yenye pointi 54 (mechi 28) na Yanga waliocheza michezo 27 wakiwa na pointi 51.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*