MOURINHO, POGBA NA MABIFU MENGINE YA MAKOCHA, WACHEZAJI

LONDON, England


 

ILIANZA kama utani lakini sasa hali ni mbaya katika uhusiano wa kocha mwenye maneno mengi, Jose Mourinho na kiungo wake wa bei kali, Paul Pogba.

Vuguvugu la uhusiano mbaya kati ya wawili hao lilifikia kilele chake wiki iliyopita, baada ya kipande cha video kilichosambaa mitandaoni kikiwaonesha wawili hao wakitupiana maneno mazoezini.

Kabla ya hapo, Pogba alianza kuliamsha kwa kauli yake mbele ya waandishi wa habari baada ya sare ya bao 1-1 na Wolves, mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa katika Uwanja wa Old Trafford.

Katika kile kilichoonekana ni kuzikosoa mbinu za Mourinho za kupaki basi, Pogba alisema Man United inatakiwa kushambulia, hasa inapokuwa nyumbani na ndiyo utamaduni wa timu hiyo.

Aidha, hali ya mvutano wao imeibua shaka kuwa kuna uwezekano wa Pogba kuondoka klabuni hapo, ambapo klabu za PSG, Juventus na Barcelona zimekuwa mstari wa mbele kuisikiliza saini yake.

Hata hivyo, ulimwengu wa kandanda unatambua kuwa hiyo si mara ya kwanza kuwashuhudia makocha na wachezaji wao wakiingia kwenye ‘bifu’ kwani imewahi kutokea mara kadhaa huko nyuma.

Raymond Domenech vs Anelka (Ufaransa)

Moja kati ya bifu kali la kocha na mchezaji wake. Tatizo lilianzia pale Nicholaus Anelka alipomponda kocha huyo baada ya mchezo waliopoteza dhidi ya Mexico, katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 huko Afrika Kusini.

Kitendo hicho cha Anelka kumpa makavu mbele ya waandishi wa habari kilimkera kocha Domenech na uamuzi wake ulikuwa ni kumrejesha nyumbani nyota huyo wa zamani wa Chelsea na Arsenal.

Roberto Mancini vs Carlos Tevez (Man City)

Wawili hao waliingia katika uhasama msimu wa 2011-12 walipokuwa Man City. Kisa kilikuwa ni Tevez kukataa kutokea benchi zikiwa zimebaki dakika chache kabla ya kumalizika kwa mtanange wao dhidi ya Bayern Munich.

Kuanzia hapo wawili hao wakawa ‘chui na paka’ na msimu mmoja baadaye, Tevez alinyoosha mikono na kutimkia zake Juventus. Hiyo ilikuwa mwaka 2013.

Alex Ferguson vs David Beckham

Inaelezwa kuwa kama si bifu hilo basi huenda Beckham asingeondoka Manchester United mwaka 2003 na kwenda Hispania kujiunga na wababe wa soka la nchi hiyo, Real Madrid.

Ferguson hakuwa akifurahishwa na mwenendo wa Beckham hasa matukio yake ya nje ya uwanja, ambapo staa huyo alikuwa akipenda maisha ya kuzungumziwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari.

Tukio kubwa lililothibitisha kuwa wawili hao ni maadui ni lile la mzee Ferguson kumrushia kiatu Beckham wakiwa kwenye chumba cha kubadilishia.

Graeme Souness v Craig Bellamy

Kwa wafuatiliaji wa muda mrefu wa Ligi Kuu ya England, wanamjua Belllamy kwa mambo makubwa mawili. Kwanza, mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool alikuwa straika hatari kwa kipa yeyote. Pili, alikuwa mkorofi wa kiwango kizuri tu.

Licha ya kwamba amewahi kukorofishana mara kadhaa na wachezaji wenzake, ugomvi wake ‘bab kubwa’ ni ule na aliyekuwa kocha wa Newcastle kipindi hicho, Graeme Souness.

Bifu lilianza mwaka 2005 na kisa kilikuwa ni kocha Souness kumtaka Bellamy acheze winga ya kulia, jambo ambalo nyota huyo alilikataa kwa kisingizio cha majeraha.

Utovu huo wa nidhamu ulimfanya ang’olewe kikosi cha kwanza na adhabu haikuishia hapo, akatozwa faini ya Pauni 80,000. Wiki chache baadaye, Bellamy alimkoromea msaidi wa Souness, John Carver.

Ruud Gullit v Alan Shearer

Kama inavyoweza kuwa sababu ya Mourinho na Pogba kutofautiana, Gullit aliyekuwa akiinoa Newcastle hakutaka kujishusha kwa Shearer ambaye ukweli ni kwamba kipindi hicho ndiye aliyekuwa roho ya timu hiyo.

Ikizingatiwa kuwa kabla ya kuingia katika kazi ya ukocha, Gullit alikuwa na jina kubwa Uholanzi kutokana na mafanikio yake akiwa na timu yake hiyo ya taifa, hakuona sababu ya ‘kumsujudia’ Shearer kama walivyokuwa wakifanya viongozi na mashabiki wa Newcastle.

Uamuzi wake mkubwa ulioibua shaka kuwa hamkubali straika huyo ni ule wa kumweka nje katika mchezo waliotandikwa mabao 2-1 na Sunderland katika msimu wa 1999/2000.

Mashabiki walichukizwa na hatua hiyo ya Gullit kumweka benchi mfalme wao na haikuchukua muda mrefu kabla ya kocha huyo kufukuzwa, ambapo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ‘Shearer ni mchezaji anayesifiwa zaidi kuliko uwezo alionao’.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*