MOURINHO AWAJIA JUU WANAODAI KAWAPA UBINGWA MAN CITY

LONDON, England   |

KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba jitihada zilizofanywa na Manchester City msimu mzima ndio sababu ilyowawezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England na wala si kipigo ambacho Manchester United walikapata juzi dhidi ya West Brom.

Wiki mbili zilizopita Man United waliweza kuonesha ubora wa hali ya juu dhidi ya kikosi hicho cha Pep Guardiola na kufanikiwa kuzima sherehe zao, lakini juzi wakajikuta wakiambulia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa timu ambayo inashika mkia ya Baggies na hivyo kuwafanya majirani zao kukabidhiwa taji hilo kwa mara ya tatu.

Kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya wanaodai kuwa kipigo hicho ndicho kilichowafanya Man City watwae ubingwa, jambo ambalo linakanushwa vikali na Mourinho na huku akiwataka wanaozusha kuachana naye.

Akizungumza katika mahojiano na Sky Sports, Mreno huyo alisema kuwa mara zote huwa hafurahishwi kuona mtu anasema ametwaa ubingwa baada ya mwenzake kufungwa.

“Nimewahi kutwaa ubingwa. Na mara zote huwa sifurahishwi wakati mtu mwingine anaposema nimetwaa ubingwa kwa sababu mtu mwingine amefungwa,”  alisema Mourinho.

“Manchester City wamefanikiwa kutwaa ubingwa kwa sababu walikuwa na pointi nyingi kuliko timu yoyote. Huwezi kusema kwamba Manchester City wametwaa ubingwa kwa sababu Manchester United walipoteza mechi yao,”    aliongeza Mourinho.

Ushindi huo kwa upande wa West Brom umekuja katika mchezo wa pili tangu kocha wao wa  muda, Darren Moore akabidhiwe mikoba na kocha huyo mwenye umri wa miaka 43, anaamini umoja alioujenga ndiyo sababu kubwa kumaliza kipindi hicho kigumu kwao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*