MOURINHO AWABEZA MAN CITY KWA UBINGWA

LONDON,   England

KWA kile ambacho unaweza kusema  ni kama amewabeza, Kocha  Jose Mourinho amewatumia salamu za kuwapongeza  Manchester City  kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, licha ya kuwatibulia sherehe zao walizoziandaa  katika Uwanja wa  Etihad.

Kabla ya mchezo huo wa juzi, baadhi ya mashabiki wa timu hiyo walikuwa wameshajiandaa kushangilia ubingwa kutokana na kuwa walikuwa na uhakika wa kuondoka na ushindi.

Matumaini hayo yaliongezeka zaidi baada ya Man City kupata mabao mawili ya kuongoza ndani ya dakika 30 za kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, mabao mawili yaliyofungwa na kiungo mshambuliaji wa Man Utd, Paul Pogba kipindi cha pili, ndiyo yaliyotibua sherehe hizo za Man City za kutwaa ubingwa  huku ikiwa ina mechi sita mkononi.

Alikuwa ni nyota  mkongwe wa Man City, Vincent Kompany, aliyeipatia timu hiyo bao la kuongoza kwa mpira wa kichwa mapema kipindi cha kwanza na kisha Ilkay Gundogan akaongeza la pili dakika tano baadaye kabla ya  Pogba kuyapindua matokeo hayo.

Chris Smalling  ndiye aliyeinyima bao  la ushindi Man City dakika ya  69 na hivyo kuifanya iambulie kipigo cha pili mfululizo ikiwa nyumbani, baada ya kuchapwa mabao  3-0  dhidi ya  Liverpool  katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliopigwa Jumatano wiki iliyopita.

Kutokana na matokeo hayo, Man City itawabidi kusubiri hadi Jumamosi, lakini nako inabidi waichape Tottenham na huku wakiomba Manchester United nao wafungwe na West Brom siku inayofuata.

“Mapambano yetu si kumaliza ligi tukiwa nafasi ya pili, lakini ningependa kuwapongeza Man City kwa ubingwa wanaoelekea kuutwaa na wanaustahili,”     Mourinho aliiambia Sky Sport.

“Hawawezi kuwapa wengine nafasi kwa sababu msimu huu ni wa kwao kwa vile wamekuwa wakishinda mfululizo. Na lengo langu lilikuwa ni kupata pointi na sio kuzima sherehe za watu  na pointi hizi zinaweza kutufanya tuwafikie msimu ujao,” aliongeza kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*