MOURINHO AFUKUZWE MAN UNITED?

MANCHESTER, England


KOCHA wa Manchester United, Jose Mourinho, lazima afukuzwe mara moja.

Hayo ni mawazo ya mchezaji wa zamani wa klabu hiyo ya Old Trafford, Paul Parker, ambaye anaamini inatosha sasa.

Kocha huyo maarufu kwa jina la Special One, amekuwa kwenye presha kubwa katika wiki hizi mbili baada ya kuanza vibaya msimu huu wa Ligi Kuu England.

Hii inafuata baada ya kuwa na maandalizi mabaya ya msimu mpya ambapo Mourinho aligombana na bodi yake ya timu kuhusu suala ya usajili, akiwaponda mabosi wake hadharani juu ya masuala hayo.

Timu hiyo ya Red Devils imepoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ikiwamo ya mwanzoni mwa wiki hii dhidi ya Tottenham kwa kuchapwa nyumbani Old Trafford kwa mabao 3-0 na ile ya Brighton, ambayo walipigwa 3-2.

Kipigo hicho cha kocha huyo wa zamani wa Chelsea amepoteza kwa kufungwa mabao mengi kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa nyumbani na kushindwa kujizuia.

Na Parker anaamini kwamba, huu ndio wakati wa kufanya mabadiliko Old Trafford.

“Soka limekuwa bovu mno,” anasema Parker akizungumza na mtandao wao talkSPORT.

“Kiwango kimekuwa kibovu ila kuna watu kibao wamekaa wanasema ni mshindi na hilo ni suala la ushindi. Manchester United si klabu ya kushinda tu. Ni timu ya staili, mbinu za ushindi. Pia ni timu ya swaga.

“Kwa sasa timu hiyo haifanyi hivyo kabisa. Hayo mambo hayapo tena, imekuwa kama timu ambayo haina kocha.

“Hakuna kule kujielezea tena, hawashawishi tena. Ed Woodward anapaswa kumfukuza Jose Mourinho. Unawalipa wachezaji mamilioni kwa mamilioni na bado unashindwa kuwadhibiti wachezaji. Huo ni ujinga kwa klabu kama Manchester United,” anaongeza Parker.

“Mwisho wa siku mabadiliko yanahitajika Manchester United, staili yao ya uchezaji haiwezi kubadilika wakati Jose Mourinho akiendelea kuwapo kwenye timu. Ni njia ambayo makocha wanawashusha viwango wachezaji.”


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*