googleAds

Molinga, Mustafa hakijaeleweka Yanga

NA WINFRIDA MTOI

LESENI za wachezaji wa Yanga, David Molinga na Seleman Mustafa, vimeendelea kuutoa jasho uongozi wa klabu hiyo, unaohaha kuzipata kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Molinga aliyesajiliwa na Yanga kutoka FC Lupopo na Mustafa kutoka Burundi, wameshindwa kucheza mechi za mashindano za timu hiyo kutokana na kikwazo hicho.

Hamu ya mashabiki wa Wanajangwani hao, kutaka kuwaona wachezaji hao katika mechi za Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, imewafanya viongozi wa Yanga kuhangaika kupata vibali hivyo.

Akizungumza na DIMBA Jumatano jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema wanaendelea kushughulikia suala hilo na wapo katika hatua nzuri, muda wowote watavipata.

Mwakalebela alisema, kama walivyofanikiwa kupata leseni ya  Farouk Shikalo, wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha hata Molinga na Mustafa wanapata, kwa sababu ni wachezaji muhumu katika kikosi hicho.

“Shikalo tayari leseni yake ya CAF amepata, ni mwalimu mwenyewe kuamua kumchezesha katika mechi ijayo dhidi ya Zesco, kuhusu Molinga na Mustafa tunaendelea kufuatilia, naamini haitachukua muda mrefu,” alisema Mwakalebela.

Katika hatua nyingine, Makamu huyo Mwenyekiti alisema wameshamalizana na beki wao Andrew Vincent ‘Dante’ ambaye sasa ataungana na wenzake wakati timu itakapowasili jijini Dar es Salaam ikitokea Mwanza.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*