googleAds

Mo Rashid atema cheche

NA MOHAMED KASSARA

MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Mohamed Rashid ‘Mo Rashid’, amesema atatumia muda wa mapumziko ya Ligi Kuu Tanzania Bara kupisha michuano ya Kombe la Chalenji kujifua vikali kwa lengo la kurudi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Rashid alijiunga na JKT Tanzania kwa mkopo mwanzoni mwa msimu huu, akitokea Simba iliyomsajili misimu miwili iliyopita kutoka Tanzania Prisons ya Mbeya.

Mchezaji huyo amepoteza nafasi kwenye kikosi hicho mbele ya Dany Lyanga na Abdurahman Mussa ambao wamekuwa wakianza mara kwa mara chini ya kocha Abdallah Mohamed ‘Bares’.

Akizungumza na BINGWA jana, Rashid alisema atahakikisha anatumia muda huo wa mapumziko ya ligi kujiweka fiti ili kimshawishi kocha kumwanzisha katika kikosi chake michezo zijazo.

“Siridhishwi na kiwango changu cha hivi sasa, napambana kuhakikisha narudi katika makali niliyokuwa nayo Prisons, nipo kwenye timu yenye changamoto ya namba, ushindani umekuwa mkubwa kwangu, nimepanga kutumia muda huu wa mapumziko kujifua kivyangu ili kujaribu kurudisha mabao yangu.

“Maisha yana changamoto nyingi, lakini kikubwa ni kupambana ili kuzivuka, naamini nitarudi kikosi kama nitakuwa kwenye ubora wangu, kwa sasa acha nikomae na mazoezi binafsi ili kujiweka fiti zaidi,” alisema mpachika mabao huyo wa zamani wa African Sports ya Tanga.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*