MO Dewji asisitiza uwekezaji zaidi Simba

LULU RINGO, DAR ES SALAAM

Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘MO Dewji’ amesema klabu hiyo inahitaji kuwekeza zaidi ili iweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ikiwemo kumiliki wachezaji wenye uwezo mkubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa, Februari 8, 2019 MO Dewji amekiri Simba kushindwa kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 10 katika michezo miwili mfululizo dhidi ya AS Vita ya Algeria na Al Ahly ya Misri.

Amesema timu ambazo Simba zimekutana nazo zina uwekezaji mkubwa katika soka na pia zina uzoefu mkubwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunashindana na klabu zenye bajeti kubwa na uzoefu mkubwa katika michuano ya kimataifa, unapoizungumzia Al Ahly ni sawa na kuizungumzia Real Madrid (ya Hispania) katika kutwaa mataji, juzi nimesikia wamenunua mchezaji kwa Shilingi bilioni 10, AS Vita nao mwaka jana wameshiriki fainali za Kombe la Shirikisho Afrika,” amesema MO Dewji.

Aidha MO Dewji amesema wapo wachezaji wanaoitumikia Simba lakini hawana uchungu na timu hiyo na hawana uwezo wa kushiriki katika michuano ya kimataifa.

“Ukiangalia Simba inaweza kuwa na wachezaji wanne tu wenye uwezo wa kushiriki michuano ya kimataifa, wapo wengine hawana nidhamu wala uchungu na timu. Tumepanga kuwaondoa wachezaji wasio na nidhamu pindi mikataba yao ikifika ukingoni,” aliongezea mwekezaji huyo.

Kuhusu mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly itakayochezwa Jumanne Februari 12 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, MO Dewji amewataka mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi.

Amesema wamepunguza kiingilio cha chini katika mchezo huo ambapo kitakuwa Shilingi 2,000 ili kila mtu aweze kushuhudia mtanange huo.

“Katika mpira mashabiki wananafasi kubwa sana ya kuweza kuleta matokeo chanya, nawaomba mashabiki wa Simba wasikate tamaa kutokana na matokeo yaliyopita, wajitokeze kwa wingi uwanjani kuishangilia timu yao, tunahitaji alama tatu ili tujiweke katika nafasi nzuri ya kushinda,” amesema.

Simba ilipoteza dhidi ya Al Ahly katika mchezo wa kwanza baada ya kukubali kichapo cha mabao 5-0 mchezo uliopigwa nchini Misri Jumamosi Februari 2, 2019.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*