googleAds

MO Dewji ambakiza Manara Simba

NA MWANDISHI WETU

ZIKIWA zimebaki wiki mbili kabla ya Ofisa Habari mpya wa klabu ya Simba, Gift Macha aanze majukumu yake, imefahamika kuwa nafasi hiyo imeota mbawa baada ya Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mohamed Dewji ‘MO’ kuamua Haji Manara aendelee na majukumu yake.

Chanzo maalum kutoka ndani ya Bodi hiyo kimesema kuwa wamefuta ujio wa Macha, hivyo Manara ataendelea kushika nafasi hiyo ambayo sasa ana zaidi ya miaka minne toka Mei mwaka 2015.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu huyo wa uhakika, MO amewajulisha wajumbe kuwa Manara anaendelea kushika nafasi yake na hakuna mabadiliko katika nafasi hiyo ambayo ilitangazwa na waliyoomba walifanya usaili wa kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, Macha alisema yeye aliomba nafasi ya Ofisa Habari wa klabu ya Simba, alichokuwa akisubiri ni kupata taarifa ya kuwa amepitishwa au la na mpaka jana hakuna taarifa inayohusu kwenda kwake kuanza kazi Simba.

“Sina ninachojua kuhusu kwenda Simba au kubaki Azam TV, kama kuna nafasi hiyo nitajulishwa ila nipo kwenye kituo changu cha kazi naendelea na majukumu yangu hapa Azam,” alisema Macha.

Bingwa lilimtafuta Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Swedi Mkwabi kuzungumzia hilo na kusema yupo mkoani Tanga, hana taarifa yoyote kuhusu hiyo ya Ofisa Habari.

Alisema anachojua kuna watu wenye kujumu hilo la kukamilisha mtu atayeshika nafasi hiyo kama utaratibu unavyotakiwa.

Mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugezi (jina tunalo), alisema kuwa taarifa rasmi kama Manara anaendelea au iwapo kuna mabadiliko ya nafasi hiyo, itawekwa wazi muda wowote kuanzia sasa.

Alisema licha ya kusikia kuna taarifa za kuendelea kwa Manara katika nafasi hiyo yeye kwake ni vigumu kuzungumzia moja kwa moja.

Hivi karibuni, Manara zaidi ya mara mbili alikuwa aitishe mikutano na waandishi wa habari, lengo likiwa ni kutaka kujitoa ndani ya klabu hiyo, aendelee kufanya majukumu yake mingine nje ya klabu ya Simba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*