MKWASSA AIFUMUA YANGA

ZAINAB IDDY NA TIMA SIKILO

KIKOSI cha kwanza cha Yanga kinachotarajiwa kuivaa Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo, kitakuwa na sura mpya kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na kocha wa muda, Charles Boniface Mkwassa ‘Master’.

Mkwassa aliyekabidhiwa timu baada ya kutimuliwa kwa Mwinyi Zahera, mchezo huo wa leo ni wa kwanza kwake tangu alipopewa majukumu hayo, akiwa amepania kuvuna pointi zote tangu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.

Katika mazoezi yake ya kwanza jana asubuhi kwenye uwanja huo, aliwapanga pamoja wachezaji 11 wanaotarajiwa kuanza leo, akiwamo Rafael Daudi ambaye hakuwa akipewa nafasi sana na Zahera.

Mbali ya Daudi anayetarajiwa kucheza nafasi ya kiungo, pia kuna Japhary Mohammed ambaye naye anapewa nafasi kubwa kuanza kama beki wa kushoto.

Pia, Juma Balinya na Patrick Sibomana, wanatarajiwa kuungana na David Molinga kuunda safu ya ushambuliaji, huku Mrisho Ngassa akianzia benchi, wakati Deus Kaseke akitangulia dimbani.

Kutokana na mazoezi hayo ya jana, kikosi cha kwanza cha Yanga kinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo; 

Kipa ni Farouk Shikalo, beki wa kulia Juma Abdul, Japhary Mohammed (kushoto), wakati mabeki wa kati ni Kelvin Yondani na Ally Mtoni ‘Sonso’.

Viungo ni Rafael Daudi, Deus Kaseke na Papy Tshishimbi, wakati washambuliaji ni Juma Balinya, David Molinga na Patrick Sibomana.

Akizungumza na BINGWA kuelekea mchezo huo, Mkwassa alisema kuwa kabla ya kuanza safari ya Mtwara, alizungumza na wachezaji kabla ya kufanya hivyo tena baada ya mazoezi ya jana asubuhi Nangwanda Sijaona.

“Niliwaambia yaliotokea tuwaachie viongozi, wao na mimi tufanye kazi iliyotukutanisha ambayo ni kuisaidia timu ipate ushindi ingawa najua kwa yanayoendelea, yanaweza kutuyumbisha.

“Nimepata nafasi kumjua kila mmoja pamoja na kufahamu natakiwa kufanya jambo gani kuirejesha Yanga katika ubora pamoja na kuwafanya wote kuwa wamoja na si jambo linguine, bali kupanga timu itakayotupa ushindi tu.

“Kesho (leo) utakuwa ni mchezo kwa kwanza kwangu, nitapanga kikosi kitakachoweza kushambulia zaidi ili tupate matokeo ya ushindi. Naomba mashabiki waje kutuunga mkono kwani wao ndio watakoongeza hamasa kwa wachezaji katika kutimiza majukumu yao,” alisema Mkwassa.

Mkwassa ni muumini wa soka la kushambulia, akikumbukwa jinsi alivyoiongoza Yanga kuichapa Ruvu Shooting mabao 7-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, Februari mwaka 2014, wakati huo akiwa kocha msaidizi wa Hans van der Pluijm.

Hivyo kwa mpango wake huo wa kucheza soka la kushambulia dhidi ya Ndanda FC leo, ni wazi anataka kuona kama anaweza kuanza kurejesha dozi zao za kuanzia mabao matano na kuendelea.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*