MKWASA ATOKA ‘ICU’ INDIA

NA ZAITUNI KIBWANA


 

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Boniface Mkwasa ‘Master’, ametolewa chumba cha uangalizi maalum (ICU), baada ya hali yake kuendelea vizuri, anapotibiwa nchini India.

Mkwasa amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo kutokana na kusumbuliwa na tatizo la upumuaji.

Akizungumza na BINGWA jana, mke wa Mkwasa, Betty Mkwasa, alisema kuwa kwa sasa hali ya mumewe imeimarika baada ya kutolewa ‘ICU’ na amewekwa wodi ya kawaida tofauti na awali alivyokuwa huko.

“Mwanzo alikuwa ‘ICU’ hali yake haikuwa nzuri sana hasa baada ya kufanyiwa upasuaji, nashukuru Mungu naomba muendelee kumuombea mume wangu,” alisema.

Mkwasa alitangaza kuachia ngazi Yanga kama Katibu Mkuu hivi karibuni, akisema hawezi kuendelea kuitumikia Yanga ili kulinda afya yake.

Mchezaji huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, alitangazwa kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Febuari 1, 2007, kujaza nafasi iliyoachwa wazi kwa muda mrefu na kukaimiwa na Baraka Deusdetit baada ya kuondoka kwa Dk. Jonas Tiboroha.

Mkwasa alipata kuichezea Yanga kwa mafanikio makubwa na aliwahi pia kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo kabla ya kuwa kocha wa Taifa Stars.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*