googleAds

Mingange apigia Azam hesabu kali

NA WINFRIDA MTOI

KOCHA  wa kikosi cha  Ndanda, Meja Mstaafu wa Jeshi, Abdul Mingange, amesema anautazama mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi Azam kwa jicho la tofauti kutokana na kulifahamu benchi la ufundi la timu hiyo.

Meja Mingange aliwahi kuifundisha Azam baada ya kutimuliwa kwa Hans Pluijm  na kesho atakutana na timu hiyo, ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara, safari hii akiwa na kikosi cha Ndanda.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona,  mkoani Mtwara huku Ndanda wakitoka kushinda bao 1-0 dhidi ya Singida United na Azam wakipigwa mabao 2-1 na Coastal Union.

Akizungumza na BINGWA jana kwa simu kutoka Mtwara,  Meja Mingange, alisema mchezo huo utakuwa ni mgumu kuliko watu wanavyofikiria, ikizingatia Azam wametoka kupoteza.

Alisema anaifahamu Azam, lakini na wao wanamfahamu, kikubwa ni kujipanga wakijua wanakwenda kukutana na kocha mwenye mbinu za aina gani.

“Kati ya mchezo ninaoutazama kwa jicho la kipekee ni ule tunaokutana na Azam, wale watu wananijua na pia wana kikosi bora tofauti na timu tulizokutana nazo hivi karibuni,” alisema.

Meja Mingange alisema wanaendelea kufanya maandalizi mazuri na atamkosa mshambuliaji wake Omary Mponda ambaye anauguza jeruhi.

“Mponda tulimuacha Mtwara tulipokwenda katika mechi za Kanda ya Ziwa kwa sababu aliumia na kutakiwa kupumzika, hata kama ataanza mazoezi sitamtumia ili hali yake iendelee kuimarika,” alisema.

Ndanda inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi 22, wakati Azam ikiwa ya pili kwa pointi 44.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*