Mgunda alaumu wachezaji wake kurudia makosa

NA OSCAR ASSENGA, TANGA

KOCHA Mkuu wa timu ya Coastal Union, Juma Mgunda, amesema makosa ya kujirudia yaliyofanywa na wachezaji wake ndicho chanzo cha kupoteza mechi yao ya ligi dhidi ya Simba.

Mgunda aliyasema hayo juzi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, mara baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Simba ambayo ilimalizika kwa kipigo cha mabao 2-1.

Alisema wachezaji wake walijitahidi kupambana kuhakikisha wanapata ushindi, lakini mambo yalibadilika.

Coastal Union walipata bao dakika ya kwanza lililofungwa na Raizin Hafidh, lakini mabao mawili yaliyopachikwa na Meddie Kagere kipindi cha pili yalitosha kuipa Simba ushindi.

“Tumejitahidi sana, niliwaambia kwamba wanacheza na timu yenye watu wapo juu hivyo wawe makini sana, lakini makosa tuliyoyafanya ya kujirudia rudia tumeadhibiwa,” alisema Kocha Mgunda.

Kocha huyo alisema kwa sasa wanafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo ili mechi inayofuata wapate matokeo mazuri.

Alisema Ligi Kuu Bara msimu huu umekuwa ngumu na utaendelea kuwa hivyo kwasababu kuna timu zinapambana kutokushuka daraja na nyingine kupata ubingwa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*