googleAds

Mghana azua jambo, Msuva atajwa

NA WINFRIDA MTOI

YALE mavitu aliyoyafanya nyota mpya wa Yanga raia wa Ghana, Benard Morrison, katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Stand United, hayajapita hivi hivi unaambiwa.

Morrison, kiungo wa pembeni, alikuwa moto wa kuotea mbali, akigusa mpira katika mabao yote wakati Yanga wakitangaza hali ya hatari kwa ushindi wa mabao 3-1.

Tangu msimu huu umeanza, Wanayanga hawana furaha kama ilivyo kwa watani zao Simba, ambao wamekaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa muda mrefu bila kushushwa.

Kati ya maeneo yaliyokuwa yakiwaumiza vichwa ni ushambuliaji, hivyo uongozi wa Yanga kwa kushirikiana na wadhamini wao, kulazimika kuingia msituni kusaka nyota wapya kipindi cha dirisha dogo.

Kwa kiwango alichokionesha Morrison kwa mabeki wa Singida United, mchezaji huyo wa zamani wa Motema Pembe amethibitisha kuwa mabosi wa Yanga ‘hawakubugi’ kuifuata saini yake.

Wakati huo huo, unaweza kusema sasa mashabiki wa Yanga wameshatupilia mbali hasira walizokuwanazo baada ya kocha Luc Eymael kuanza  kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Kagera Sugar, kisha kulambwa bao 1-0 na Azam FC.

Kiwango kilichooneshwa na Morrison kimemuibua winga wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’,  ambaye ameliambia BINGWA kuwa wamepata kile walichokuwa wanakitafuta kwa muda mrefu Jangwani.

Alisema tangu ameondoka Simon Msuva, Yanga haikupata mchezaji wa aina hiyo, ambaye anaendana na falsafa ya kikosi hicho iliyozoeleka kwa miaka mingi.

“Nilivyomuaona Morrison, ni mechi moja,  lakini kuna kitu anacho na kitaisaidia Yanga kama ataendelea kucheza kwa kiwango hicho kwa sababu anaendana kabisa na falsafa ya Yanga.

“Huyu mchezaji amekuja na vitu alivyokuwa navyo Ngasa zamani. Alipoondoka, akaja Simon Msuva, ambao wote waliendana vizuri na falsafa ya Yanga ya kushambulia kutoka pembeni,” alisema SMG.

SMG alisema Ngasa yupo lakini amekuwa tofauti kidogo kwa sababu hafanyi vitu vyake kama ilivyokuwa zamani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*